WAZIRI MKUU LESOTHO ATAKIWA KUTANGAZA MATOKEO YA TUME YA SADC
KIKAO maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na
Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC Double Troika) kimeiagiza Serikali ya Lesotho iwe imetangaza
matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa nchini humo
ifikapo Februari Mosi, mwaka huu.
Agizo hilo lililotolewa kwa Waziri Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha
Mosisili katika kikao cha SADC Double Troika kilichofanyika mapema wiki
hii Gaberone, Botswana, chini ya Mwenyekiti wake, Luteni Jenerali
Seretse Khama Ian Khama ambaye pia ni Rais wa nchi hiyo.
SADC Double Troika ni kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC
Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama
(SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation)
kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini
Gaborone, Botswana.
Pamoja na kutaka Lesotho itangaze matokeo ya tume hiyo, SADC Double
Troika iliitaka nchi hiyo iandae mchakato wa kueleza njia za utekelezaji
wa mageuzi kama yalivyopendekezwa kwenye ripoti ya tume hiyo ifikapo
Agosti, mwaka huu.
“Vilevile, nchi ya Lesotho inatakiwa kuandaa mazingira wezeshi
yatakayotoa nafasi kwa viongozi wa upinzani na baadhi ya maofisa wa
kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko, waweze kurejea
nyumbani,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na sekretariati ya SADC
siku moja baada ya kikao hicho kumalizika.
Mkutano huo wa Botswana ulihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli; Rais wa
Botswana, Luteni Jenerali Khama; Rais wa Afrika Kusini, Bw. Jacob Zuma;
Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto Nyusi; Waziri Mkuu wa Swaziland,
Dk. Barnabas Dlamini na Waziri wa Mambo wa Nje wa Zimbabwe, Bw.
Simbarashe Mumbengegwi ambaye alimwakilisha Rais Robert Mugabe wa nchi
hiyo.
SADC Double Troika ni mkutano unaohusisha viongozi wakuu watatu
wanaoongoza chombo cha ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama na
wengine watatu kutoka kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC.
Hawa wanawakilisha mwenyekiti aliyepo madarakani, mwenyekiti
aliyemaliza muda wake na mwenyekiti ajaye ambaye huwa ni makamu
mwenyekiti.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Balozi Radhia
Msuya, chini ya muundo wa SADC, kuna mambo makuu mawili; la kwanza
likiwa ni utangamano wa kikanda ambao unasimamiwa na mkutano wa wakuu wa
nchi (SADC Summit) na la pili ni la siasa, ulinzi na usalama ambalo
linasimamiwa na chombo maalum (SADC Organ).
Akifafanua zaidi, Balozi Msuya alisema wajumbe wa mkutano wa SADC Organ
ni Msumbiji (Mwenyekiti); Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda
wake) na Tanzania inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo
Agosti, 2016. Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaundaSADC
Summit.
Mapema, kikao hicho, kilipokea taarifa ya msuluhishi wa SADC kwenye
mgogoro wa Lesotho ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Dk.
Cyril Ramaphosa ambayo iliainisha mambo kadhaa yakiwemo ya kikatiba na
kiusalama ndani ya nchi hiyo.
Dk. Ramaphosa alitakiwa kuhakikisha kuwa mgogoro huo uliovihusisha
vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi ya Lesotho, unatatuliwa kwa njia
ya mazungumzo kati ya wadau husika ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo
inarudi kwenye hali ya amani – kisiasa na kiusalama.
Mgogoro wa Lesotho umehusisha kuuawa kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya
Lesotho, Luteni. Jenerali Maaparankoe Mahao, mnamo Juni 25, 2015. Pia
baadhi ya wananchi wanadaiwa kutiwa vizuizini na wengine kuwekwa ndani.
No comments:
Post a Comment