SERIKALI YAANZA UTEKELEZAJI WA RUZUKU YA PEMBEJEO ZA KILIMO KWA NJIA YA VOCHA.
Msemaji
wa Wizara ya Kilimo cha Chakula na Ushirika, Richard Yasini
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya pembejeo za
kilimo zenye thamani zaidi ya Sh. Bilioni 78 ambazo zimesambazwa katika
mikoa 24 ya Tanzania Bara ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na
mbegu bora katika msimu wa 2015/2016.Vocha hizo zitawanufaisha wakulima
999,926 wanaojihusisha na kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga. Mkutano
huo umefanyika leo jijini Dar es salaam kulia ni Mkurugenzi Msaidizi
wa MAELEZO, Zamaradi Kawawa.
Baadhi ya waadnishi wa habari wakimsikiliza Msemaji wa Wizara ya Kilimo cha Chakula na Ushirika, Richard Yasini.
Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.
Na. Georgina Misama - MAELEZO
WAKULIMA
wapatao milioni moja wameanza kunufaika na usambazaji wa vocha za
pembejeo za kilimo ambazo Serikali inazitolea ruzuku kwa ajili ya
wakulima katika mikoa 24 ya Tanzania bara (ukitoa mkoa wa Dar es Salaam)
ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora kwa mwaka
2015/2016.
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw.
Richard Kasuga amesema kwamba pembejeo za kilimo zenye thamani ya zaidi
ya shilingi bilioni 78 zitawanufaisha wakulima wanaojishughulisha na
kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga.
“Usambazaji
wa vocha hizo umeshaanza, Serikali kwa kushirikiana na makampuni 23 ya
mbolea na 27 ya mbegu bora ya mahindi na mpunga yanaendelea kutoa
huduma ya usambazaji wa pembejeo katika mikoa husika” amesema Bw
Kasuga.
Bw.
Kasuga amesema kwamba ili kuhakikisha mbolea na pembejeo zinatumika
ipasavyo, Serikali inatekeleza jukumu hilo kwa kugawa majukumu kwa ngazi
mbalimbali ikianza na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kamati ya
Taifa ya Uendeshaji wa Utaratibu wa Vocha, Mikoa, Wilaya, Kata mpaka
Vijiji.
Akijibu
swali la mwandishi aliyetaka kujua Serikali inafanya juhudi gani katika
kudhibiti ubora wa pembejeo hizo, Kaimu Mkurugenzi, Mamlaka ya udhibiti
wa Ubora wa Mbolea Bw. Lazaro Kitandu amesema toka kuundwa kwa Mamlaka
ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea tatizo la ubora limepungua kwa kiasi
kikubwa kwani mamlaka hiyo inasimamia zoezi zima la utengenezwaji na
usambazaji wa mbolea na pia wakulima wanapewa elimu ya matumizi sahihi
na namna bora ya kuhifadhi.
Aidha,
Serikali imetoa rai kwa wakulima kutumia ruzuku inayotolewa ili waweze
kujikomboa kiuchumi kwa kuboresha kilimo, na kuwasihi baadhi ya wakulima
wanaouza vocha zao wasidanganyike kwa kupokea hela na kuuza haki yao.
Serikali
ilianzisha utaratibu wa matumizi ya vocha mwaka 2008/2009 ili kuboresha
mfumo wa usambazaji mbejeo kwa wakulima. Utaratibu huu umesaidia
kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, hivyo Taifa kufaidika na
kujitosheleza kwa chakula.
No comments:
Post a Comment