HOTUBA YA WAZIRI MKUU PINDA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA 18 WA BUNGE
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO
WA 18 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 7 FEBRUARI, 2015
I: UTANGULIZI
(a) Masuala ya jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Tumekuwepo
hapa kwa takriban siku 12 katika shughuli za Mkutano wa 18 wa Bunge
lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa
Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
2. Lakini
tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia mabadiliko katika Baraza la
Mawaziri na Wenyeviti wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge. Niruhusu
nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote
ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika mabadiliko hayo.
Aidha, napenda niwapongeze Wenyeviti watatu pamoja na Makamu mmoja kwa
kuchaguliwa kuongoza Kamati za Kudumu za Bunge ikiwemo Kamati ya Bajeti,
Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Tunawatakia afya njema Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wenyeviti wote katika
kutekeleza majukumu yao mapya.
Mheshimiwa Spika,
3. Tangu
tulipomaliza Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge lako Tukufu, kumetokea
majanga katika sehemu mbalimbali Nchini ikiwemo mafuriko na mapigano ya
Wakulima na Wafugaji kule Morogoro, pamoja na ajali za barabarani.
Naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wote walioathirika na majanga,
maafa na ajali za barabarani. Kwa wale waliopoteza maisha tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi Amina.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo
papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 15 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
(c) Miswada na Taarifa Mbalimbali
Mheshimiwa Spika,
5. Tunahitimisha
Mkutano huu tukiwa tumekamilisha kazi kubwa ya kusoma na kujadili
taarifa mbalimbli za Kamati za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta.
Kamati za Kisekta ambazo Taarifa zake zimewasilishwa na kujadiliwa na
Waheshimiwa Wabunge ni zifuatazo:
i) Kamati ya Miundombinu;
ii) Kamati ya Nishati na Madini;
iii) Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira;
iv) Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji;
v) Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala;
vi) Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
vii) Kamati ya Masuala ya UKIMWI;
viii) Kamati ya Ulinzi na Usalama;
ix) Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
x) Kamati ya Huduma na Jamii; na
xi) Kamati ya Maendeleo ya Jamii.
6. Aidha, Bunge Lako Tukufu lilipokea na kujadili Taarifa za Kamati zisizo za Kisekta zinazosimamia Fedha za Umma zifuatazo:
i) Kamati ya Hesabu za Serikali;
ii) Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa; na
iii) Kamati za Bajeti.
Mheshimiwa Spika,
7. Vilevile,
tumepokea na kujadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa
kuchunguza sababu za migogoro baina ya Wakulima, Wafugaji Wawekezaji na
Watumiaji wengine na Ardhi Nchini.
No comments:
Post a Comment