Header Ads

WAHISANI WA MAENDELEO KUTOKA MAREKANI WAZINDUA MIONGOZO YA KUPAMBANA NA MAGONJWA YA MAAMBUKIZI ZANZIBAR

 Mkurugenzi wa Mradi wa kudhibiti na kuzuia maambukizi ya magonjwa unaosimamiwa na Shirika la Afya la Kimataifa la Jhpiego Dkt. Albert Komba (alisimama) akitoa maelezo katika uzinduzi wa Miongozo ya kitaifa ya kukinga na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya magonjwa katika sherehe zilizofanyika Wizara ya Afya Mjini Zanzibar.
  Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib akizundua vitabu viwili vya miongozo ya Kitaifa ya kukinga  na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya magonjwa katika Hospitali na sehemu za  kutolea huduma za Afya katika sherehe zilizofanyika Wizara ya Afya Mjini Zanzibar.
 Dkt. Jamala Adam Taib akionyesha vitabu  vya miongozo ya Kitaifa ya kukinga na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya magonjwa katika Hospitali na sehemu za kutolea huduma za Afya.
 Meneja Mradi wa kudhibiti na kuzuia maambukizi ya magonjwa Zanzibar Bi. Asma Ramadhan Khamis akitoa shukrani mara baada ya uzinduzi wa Mradi huo.
Picha ya pamoja ya watendaji wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Wizara  hiyo (wa kati kati) waliokaa Dkt. Jamala Adam Taib na viongozi wa Shirika la Jhpiego baada ya uzinduzi wa miongozo ya Kitaifa ya kukinga na kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya magonjwa.(Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar).
=======  ========
NA RAMADHANI ALI/HABARI MAELEZO.
                   
Wizara ya  Afya kwa kushirikiana na wahisani wa Maendeleo kutoka Marekani na Shirika la Afya la Kimataifa la Jhpiego imezindua miongozo miwili ya Kitaifa katika kukinga na kudhibiti kuenea kwa mambukizi ya magonjwa katika Hospitali na sehemu za kutolea huduma za afya Zanzibar.

Miongozo iliyozinduliwa ni wakuboresha viwango katika Hospitali na vituo vya afya ili kuzuia na kudhibiti maambukizo  na  ule unaobainisha vigenzo vya tathmini ili hospitali ziweze kutambuliwa na kupewa tunzo zitakazobainisha jitihada za vituo katika kufikia viwango vya ubora vya kitaifa.

 Akizindua miongozo hiyo katika sherehe zilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja, Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Afya Dkt. Jmala Adam Taib amewataka madaktari na wafanyakazi wa vituo vya afya kubadilika katika kutoa huduma ili kupunguza maabukizi ya magonjwa wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa.

“Imebainika kati ya wagonjwa 100 wanaofikishwa katika Hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba, 15 kati yao wanapata magonjwa mengine  mapya wakiwa sehemu hizo jambo ambalo linaongeza gharama za matibabu kwa wagonjwa hao,”alisema Dkt. Jamala.

Ameshauri kuanzisha utaratibu utakaohakikisha maeneo ya kutolea huduma za afya  zinakinga na kudhibiti kiwango cha maambukizi ya magonjwa ili kuwalinda wananchi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na za kiwango cha juu.

“Miongozo hii isaidie kuzifanya Hospitali zetu ziwe sehemu za wagonjwa kwenda kupata huduma na sio kuishia kupata maambukizi mapya na kuwaongezea mzigo na madhara zaidi,” alisisitiza kaimu Mkurugenzi Wizara ya Afya.

Amesema kitu muhimu kwa wafanyakazi ni kushirikiana katika kuzitunza na kuziendeleza nyenzo zilizopo katika Hospitali na vituo vya afya  na kuzifanyia matengenezo ambazo haziko katika hali nzuri ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Dkt. Jamala ameongeza kuwa miongozo hiyo pia itasaidia kuwalinda watoa huduma na jamii nzima katika hatari ya kupata maambukizo wakati wakiwasaidia wagonjwa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Mradi wa kudhibiti na kuzuia maambukizo ya magonjwa unaosimamiwa na  Shirika la Jhpiego Dkt. Albert Komba ameahidi  Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuhakikisha kiwango cha maambukizo mahospitalini kinapungua.

Amewashauri wataalamu wa Afya na wafanyakazi wa Hospitali na vituo vya Afya  kutekeleza wajibu wao na kuunga mkono mpango huo  kwa vitendo na Shirika la Jhpiego litaendelea kuwajengea uwezo ili  uweze kufanikiwa.

Dkt. Albert amesema Hospitali na vituo vya Afya vya Tanzania Bara vilivyoanzisha mpango huo zimepata mafanikio makubwa na ameeleza matumaini yake kwamba Zanzibar itanufaiki zaidi katika mpango huo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Powered by Blogger.