TANZANIA YA KWANZA AFRIKA MASHARIKI KATIKA USAFIRI WA MABASI YAENDAYO KASI - PINDA
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia kwenye ubia na sekta binafsi katika mradi mkubwa wa usafirishaji abiria.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Juni 3, 2014) wakati akifungua Mkutano
wa Majadiliano yenye lengo la kuutangaza mradi wa mabasi yaendayo kasi
kwenye ukumbi wa Mlimani City. Mkutano huo wa siku mbili, utamalizika
kesho (Jumatano, Juni 4, 2014).
Waziri
Mkuu amesema kutèkelezwa kwa mradi huo kutatoa fursa za ubunifu
utakaowezesha kupatikana kwa suluhisho la usafiri mijini na hasa kwenye
miji inakua kwa kasi barani Afrika.
"Mbali
ya kutoa huduma za hali ya juu, za haraka na ambazo siyo ghali kwa
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, nia ya Serikali ni kuona mfumo mpya wa
matumizi ya kadi kwenye mpango huu wa usafiri unatumika ipasavyo,"
alisema.
Alisema
ni matumaini ya Serikali kwamba wadau kutoka sekta binafsi ambao ni
wazawa na wa kutoka nje ya nchi watashiriki kwenye mradi huu ili uweze
kuboresha matumizi ya kadi ambayo mtu hatatakiwa kulipia fedha taslimu
akiwa ndani ya basi bali kutumia kadi anayoilipia kabla ya kuingia ndani
ya basi husika.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu
alisema Serikali iliamua kuanzisha mradi huo ili kupunguza msongamano wa
magari kwenye barabara za Jiji la Dar es Salaam.
"Hii
ni awamu ya kwanza ambayo inakaribia kukamilika na inaanzia Kimara hadi
Kivukoni na itakuwa na matawi mawili ya Morocco na Karikoo. Mradi wote
una awamu sita za ujenzi kuelekea maeneo tofauti ya Jiji," alisema.
Mbali
na mradi huo wa mabasi yaendayo kasi, Serikali inaangalia uwezekano wa
kutumia usafiri wa majini kwa kutumia boti kati ya Dar es Salaam na
Bagamoyo kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar
es Salaam.
“Vilevile
tutaimarisha usafiri wa reli kama njia nyingie ya kupunguza tatizo
hili. Dk. Mwakyembe (Waziri wa Uchukuzi) ameanza na sote tumeona ni
jambo linalowezekana. Cha msingi ni kuimarisha tu usafiri huu,” aliongeza Waziri Mkuu.
Mapema,
akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia alisema Serikali imedhamiria
kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa.
Pia
alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia ambayo alisema imetoa
kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kufadhili mradi huo.
Mkutano
huo unawashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa ndani na wa nje
wanaotarajiwa kutoa huduma za mabasi makubwa na madogo, utoaji tiketi,
ulinzi, usafi na huduma za maduka.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, JUNI 3, 2014.
No comments:
Post a Comment