Header Ads

SHULE YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA VYOO




 Diwani wa kata ya Mgama Denis Lupala akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mgama wakati alipowatembelea na kula pamoja chakula cha mchana.
 Diwani wa kata ya Mgama Denis Lupala akizungumza na mwalimu mkuu wa shule hiyo Simeone Lihuluku. 
 Diwani wa kata ya Mgama, Denis Lupala akimpakulia chakula mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mgama wakati alipowatembelea na kula pamoja chakula cha mchana
baadhi ya wanafunzi shule ya sekondari ya Mgama wakiwa katika foleni ya chakula kilichoandaliwa na diwani wa kata ya Mgama Denis Lupala.


Na Denis Mlowe,Iringa

SHULE ya sekondari Mgama iliyoko katika kata ya Mgama jimbo la Kalenga wilaya ya Iringa Vijijini inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo  30 yaliyopo 12 na miundo mbinu mibovu.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wa hafla iliyoandaliwa na diwani wa kata hiyo Denis Lupala,Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Simeone Lihuluku alisema kuwa licha ya upungufu wa matundu ya choo shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa maktaba na maabara kwa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo tangu kuanzishwa kwake miaka saba iliyopita.
 
Luhuluku alisema  shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa mabweni ya wanafunzi na nyumba za kuishi walimu kitu kinachochangia wanafunzi kupanga mbali na maeneo ya shule changamoto inayosababisha ufaulu hafifu kutokana na utoro pamoja na upatikanaji wa mimba kwa watoto wa kike.

Alisema mwaka huu tayari wanafunzi watatu wamekatisha masomo kutokana na kupata ujauzito huku nyumba za walimu zinazohitajika zikiwa 18 na zilizopo kwa sasa ni nyumba mbili za walimu.
 
“Licha ya upungufu wa matundu ya vyoo vilevile tunakabiliwa na changamoto nyingi sana katika shule hii lakini kubwa zaidi ni ukosefu wa maabara na maktaba kwa ajili ya wanafunzi na tumekuwa tunatumia chumba kimoja cha darasa kama maabara kitu kinachosabisha wanafunzi kutosoma vizuri na kupunguza ufaulu naomba sana wadau waweze kuwasaidia kuondokana na changamoto hizi” alisema Lihuluku
 
Aliongeza kuwa shule hiyo imekosa huduma ya umeme,vyanzo vya kuaminika vya maji safi na vifaa vya kufundishia pamoja na uchangiaji hafifu wa michango ya shule kwa wazazi.
 
Kwa upande wao wanafunzi  wa shule hiyo wamemshukuru diwani huyo kwa kuwaandalia chakula huku wakimuomba kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika shule yao kwa lengo la kuongeza ufaulu shuleni hapo.

Shule ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa inatoa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne ikiwa na jumla ya wanafunzi 516 kati ya hao wavulana wakiwa 221 na wasichana 295 na walimu 20.

No comments:

Powered by Blogger.