Sekta binafsi yakaribisha wawekezaji wa China
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi (kushoto) akielezea jambo kwa
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Prof.
Lucian Msambichaka (katikati) na Mkurugenzi Mstaafu wa TIC na pia Balozi wa
heshima wa Botswana hapa nchini, Eng. Emmanuel Ole Naiko wakati wa kongamano la
pili la biashara kati ya Tanzania na China lililomalizika hivi karibuni jijini
Dar es Salaam.
Sekta binafsi nchini imekaribisha wawekezaji kutoka
China kuwekeza nchini kwa faida ya pande zote mbili.Akiongea na waandishi wa habari mwishoni mwa kongamano
la pili la biashara kati ya Tanzania na China Jumatano wiki hii jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Sekta Binafsi nchini (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye alisema taasisi hiyo
inakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo katika juhudi za kufikia maendeleo
endelevu hapa nchini.
“Sisi kama sekta binafsi tunasisitiza uwekezaji mzuri
unaolenga kuiendeleza Tanzania...tunawakaribisha wawekezaji hawa kuja kufanya
kazi hapa,” alisema.Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100
kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania.Hadi sasa China imesajili miradi 522 TIC yenye thamani
ya dola za Kimarekani bilioni 2.4 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 77,335.
Hata
hivyo, Bw. Simbeye aliwaambia waandishi kuwa
uwekezaji huo bado ni mdogo ukilinganisha na ukubwa wa uchumi wa taifa
hilo.“Tunahitaji uwekezaji wao ufikie dola za kimarekani bilioni
5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” alisema.Alisema sekta binafsi
inapenda waje kuwekeza zaidi
katika sekta ya viwanda na siyo kutumia fursa waliyopewa na watanzania
kuja
kuuza tu bidhaa zao.
Pia alisema wanapokuja kuwekeza ni vema wakatumia
fursa hiyo kuwasaidia watanzania kupata ujuzi na teknolojia kupitia miradi ya
ushirikiano (ubia) ili taifa liweze kupiga hatua. Alisema taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na
wawekezaji hao kutoa msaada na mwongozo wowote utakaohitajika ili kuendeleza
miradi watakayotaka kuanzisha hapa nchini.
“Tunazidi kupigania mazingira bora ya biashara ambayo
yanaendelea kuboreshwa hivyo wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie fursa
zilizopo,” alisema.Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la
Biashara (TNBC), Bw. Raymond Mbilinyi alisema Tanzania imejitahidi kwa kiasi
kikubwa kuboresha mazingira ya biashara ambayo yanavutia wawekezaji kutoka nchi
mbalimbali kuja kuwekeza kwa faifa ya nchi
na wawekezaji.“Mazingira yetu ya kufanya biashara yameboreshwa sana
na tunaendelea na juhudi kuyaboresha zaidi,” alisema.
Alisema katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano,
Tanzania inaendelea kupambana na changamoto zinazokabili mazingira ya kufanya
biashara.Alisema changamoto hizo ni pamoja na kuzidi kuboresha
mazingira ya uanzishaji biashara na upatikanaji wa ardhi ili wawekezaji
wasitumie muda mwingi.
“Maeneo mengi hayajapimwa hapa nchini,hivyo serikali
inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo ili wawekezaji wasipate usumbufu wa ardhi
ya kuwkeza,”alisema.Pia serikali inaendelea kupunguza mianya ya rushwa
ambayohuongeza gharama za kufanya biashara na kuwakatiza wawekezaji kuja
kuwekeza.
Alisema TNBC kama chombo kinachokutanisha sekta
binafsi na umma kinaendelea kuangalia kero na maeneo yanayofanya mazingira ya
biashara na uwekezaji kutokwenda vyema ili kuibadilisha Tanzania.
Kongamano hilo la siku tatu lilofunguliwa na Makamu wa
Rais wa China Bw, Li Yuanchao liliandaliwa na TIC kwa kushirikiana na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Baraza la Biashara China Afrika
(CABC) na kudhaminiwa na Stanbic Bank Tanzania.
No comments:
Post a Comment