MWENGE WA UHURU KUWASILI MKOANI SINGIDA,MAANDALIZI YAANZA
Mkuu wa Mkoa Singida Dkt. Parseko V. Kone akizungumza na
waandishi wa habari juu ya mbio za mwenge wa uhuru Mkoani Singida kulia
kwake ni katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan.
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Singida (wa
kwanza ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Geofrey Kamwela)
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone muda mfupi
kabla ya kuelekea kijiji cha Rungwa tayari kwa kuupokea Mwenge wa Uhuru
Mkoani Singida.
Wakimbiza Mwenge Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa
wa Singida Dkt. Parseko V. Kone muda mfupi kabla ya kuelekea kijiji cha
Rungwa tayari kwa kuupokea Mwenge wa Uhuru Mkoani Singida.
======== =========
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Parseko V. Kone amewataka wananchi Mkoani humo kushirikiana katika kusimamia miradi itakayowekewa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru ili thamani halisi ya fedha zitakazotumika iweze kupatikana na miradi hiyo kukamilika kwa wakati.
Dkt. Kone ametoa wito huo leo asubuhi katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2014 Mkoani Singida zitakazoanza rasmi kesho asubuhi.
Amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa katika kijiji cha Rungwa Tarafa ya Itigi Wilaya ya Manyoni ukitokea Mkoani Mbeya na utakimbizwa katika halmashauri sita za Mkoa wa Singida kisha kukabidhiwa Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Chemba kijiji cha Kinyamshindo tarehe 10 Juni 2014.
Dkt. Kone ameongeza kuwa Mwenge wa uhuru utazindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi 60 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.9 katika sekta za afya, elimu, maji, barabara, kilimo,ufugaji, ushirika,
misitu na sekta binafsi.
Aidha amewasihi wananchi kufika katika maeneo ambapo salamu za Mwenge zitatolewa ili kupata na kuuzingatia ujumbe huo. Dkt. Kone ameongeza kuwa moja ya ujumbe wa mwenge ni suala la kukamilisha mchakato wa katiba mpya huku akisisitiza wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kushiriki katika mchakato huo bila ya kuathiri umoja, amani na utulivu wa nchi yetu.
Amesema mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2014 zimebeba ujumbe usemao “Katiba ni sheria kuu ya Nchi” huku kauli mbiu ikiwa ni “Jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba Mpya” Pia ujumbe huo utaambatana na kauli za uhamasishaji jamii kupitia ujumbe wa kudumu wa Mwenge kuhusu mapambano dhidi ya Ukimwi yenye kauli mbiu isemayo “Maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi sifuri”.
Mapambano dhidi ya rushwa yatahamasishwa kwa kauli mbiu isemayo “Palipo na rushwa hakuna maendeleo” wakati huohuo kauli mbiu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya itakuwa ni “Furahia afya yako sio dawa za kulevya”.
No comments:
Post a Comment