WANAWAKE KUWENI NA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA-MAMA PINDA AASA
MKUU WA MKOA WA GEITA NA KAIMU MKUU WA
MKOA WA MWANZA SAID MAGARULA AKIMKARIBISHA
JANA 9/3/2014 MKE WA WAZIRI MKUU MAMA TUNU PINDA MKOA WA MWANAZA AMBAPO
ALIFUNGUA TAMASHA LA WANAWAKE (WOMEN DIALOGUE FRONT 2014) IKIWA NI SEHEMU YA
MAANZIMISHO YA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI YALIYOFANYIKA KATIKA HOTELI YA JB
BELMONT YA JIJINI MWANZA. HAFLA HIYO ILIYO ANDALIWA NA MIKAELA WOMEN
EMPOWERMENT INITIATIVES.PICHA PMO
============== ========== ========
MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amewaasa wanawake
nchini kwa kuwataka wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha za mikopo
wanayochukua kwa ajili kuendeshea miradi kama kweli wanataka kufanikiwa
na kutimiza malengo waliyojiwekea.
Ametoa
wito huo jana jioni (Jumapili, Machi 9, 2014) wakati akifungua Tamasha
la Wanawake (Women Dialogue Front -2014) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika kwenye hoteli ya JB Belmont,
jijini Mwanza.
Akizungumza
na washiriki wa tamasha hilo lililoandaliwa na asasi ya Mikaela Women
Empowerment Initiatives ya jijini Mwanza, Mama Tunu Pinda
alisema: “Japokuwa kwenye ujasiriamali kuna changamoto nyingi lakini
kuna wenzenu walioweza kufanikiwa. Hivyo nina imani kubwa kuwa nanyi
mtafanikiwa, ili mradi muwe na nia ya dhati katika kutekeleza malengo
mliyojiwekea.”
Akisisisitiza
haja ya kuwa na uthubutu kwenye ujasiriamali, Mama Pinda alisema:
“...Lakini niwatake wanawake wenzangu kuwa wajasiri na wenye kuthubutu
na kuwa na mipango inayotekelezeka ili muweze kutimiza ndoto zenu.”
“Sisi
wanawake tunapaswa kujitambua na kuzitumia fursa zilizopo ambazo kama
tutazizingatia ipasavyo, zitatusaidia kujenga ustawi wa maisha yetu na
jamii kwa maana kukua kwa uchumi kwa mwanamke ni kukua kwa uchumi wa
familia, kaya na jamii pia.”
Aliwataka
akinamama nchini watumie vizuri fursa za mikopo na wawe waaminifu
katika kutumia na kurejesha mikopo hiyo. “Tumieni fursa za mikopo kwa
kukopa kwa uaminifu, kimkakati na kwa malengo ili kuendeleza miradi yenu
na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Mama Tunu Pinda alisema ana imani kwamba taasisi za fedha
zitatoa kipaumbele katika kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa
wanawake wajasiriamali ili kuleta maendeleo ya kweli miongoni mwa
akinamama.
Akizungumzia
kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) katika jiji la Mwanza,
Mama Tunu Pinda aliwataka wanawake hao kuwa makini kwa kujikinga na
maambukizi mapya ya VVU kwa vile Jiji hilo lina kiwango cha juu cha
maambukizi ya ugonjwa huo.
“Utafiti
unaonyesha kwamba Jiji la Mwanza linashika nafasi ya 11 kati ya mikoa
30 ya Tanzania sawa na asilimia 4.2. Na kati ya hao wanawake ndio
wanaongoza kuliko wanaume. Hii inasababishwa na wengi wao kukosa uelewa
wa kutosha katika masuala ya afya ya UKIMWI pamoja na kukosekana kwa
usawa wa kijamii, kiuchumi na unyanyasaji wa wanawake na wasichana walio
ndani na nje ya mahusiano,” alisema Mama Pinda.
Alisema
takwimu hizo zinaonyesha ni jinsi gani mwanamke anaweza akuchukua
tahadhari mapema na ya haraka katika kupambana na ugonjwa huo hatari.
“Lakini pia mimi niseme tu, mwanamke una nafasi kubwa sana katika
kupambana na ugonjwa huu kwa kuchukua hatua za dhati na za makusudi
katika kujikinga wewe na familia yako kama mwanamke unayejitambua,”
aliongeza.
Mapema,
akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa asasi ya Mikaela
Women Empowerment Initiatives, Bibi Edith Mudogo alisema asasi hiyo
inayojishughulisha na utoaji wa mikopo midogodogo kwa akinamama, ina
jumla ya wanachama 102 ambao wanajihusisha na biashara, kilimo na
ufugaji.
Alisema
wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kunyimwa mikopo na taasisi
za kifedha kutokana na masharti yasiyo rafiki yaliyowekwa na taasisi
hizo; ukosefu wa fedha unaowanyima fursa ya kuwafikia wanawake waishio
vijijini na usumbufu unaopatikana katika kukopa na kurejesha mikopo
ingawa ni kwa kiasi kidogo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 10, 2014.
No comments:
Post a Comment