ICC:Nini hatma ya kesi ya Kenyatta?
Rais Kenyatta na wakili wa Naibu Rais William Ruto Karim Khan
Hatma
ya kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya kimataifa ya
jinai ICC, inatarajiwa kuamuliwa leo Jumatano, wakati ambapo viongozi wa
mashitaka katika mahakama hiyo wataoomba muda wa ziada kujiandaa kwa
kesi.
Mawakili wa Kenyatta wanatumai kuwa kesi hiyo ambayo imezua mgawanyiko kati ya mataifa ya Afrika itatupiliwa mbali.
Mataifa ya Afrika yamekuwa yakikosoa ICC kwa kulenga tu viongozi wa Afrika.
Kesi
dhidi ya Kenyatta ni muhimu kwa ICC ambayo imefanikiwa tu kumhukumu mtu
mmoja huku nyingi ya kesi zinazofikishwa katika mahakama hiyo
zikitupiliwa mbali kutokana na sababu nyingi tu tangu kubuniwa miaka 11
iliyopita.
Wadadisi
wanasema kuwa huenda kesi hiyo ikaleta msukosuko katika kanda ya Afrika
Mashariki ikiwa viongozi wa mashitaka watasisitiza iendelee.
Rais
Kenyatta alifikishwa ICC kutokana na tuhuma kuwa alikuwa mmoja wa
washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka
2007/2008. Anakabiliwa na makosa ya mauaji na uhalifu mwingine dhidi ya
binadamu.
Kadhalika
Kenyatta alishitakiwa pamoja na makamu wake wa Rais William Ruto kwa
tuhuma sawa. Kesi dhidi ya Ruto inaendelea katika mahakama hiyo.
Mataifa
ya Magharibi ambayo yanajitolea katika kuunga mkono ICC, pia yana
wasiwasi kuhusu uhusiano wao na Kenya ambayo inaonekana kama mshirika
mkubwa katika vita dhidi ya kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini
Somalia.
Watu
1,200 walipoteza maisha yao katika ghasia za uchaguzi mkuu mwaka 2007/08
huku maelfu wakilazimika kutoroka makwao. Wote wamekanusha mashitaka.
Viongozi
wa mashitaka ICC wanasema kuwa Kenyatta aliongoza ghasia hizo lakini
kesi dhidi yake imefanywa dhaifu kutokana na baadhi ya mashahidi
kujiondoa katika kesi hiyo tangu kesi hiyo kuwasilishwa katika mahakama
hiyo miaka minne iliyopita.
Kesi
yenyewe ilitarajiwa kuanza Jumatano, lakini ikaahirishwa kwa mara ya nne
mwezi jana wakati ambapo wendesha mashitaka waliposema kuwa shahidi
mwingine alijiondoa kwenye kesi huku wakiomba mahakama kuwapa muda zaidi
kutafuta ushahidi.
Viongozi
wa mashitaka wanasema kuwa mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa kiasi
cha kujiondoa katika kesi hiyo.Chanzo BBC Swahili
No comments:
Post a Comment