CUF itaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa

Na Hassan Hamad OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anapata haki yake inayostahiki.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ya chama hicho uliofanyika viwanja vya Kinyasini, jimbo la Chaani.
Amesema Chama hicho kitaendelea kuwa mstari wa mbele kudai mamlaka kamili ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaongozwa kwa misingi ya haki na usawa, ili wazanzibari waweze kuamua mambo yao wenyewe bila ya kuingiwa na mamlaka nyengine.
Amesifu umakini wa kamati ya Maridhiano yenye wajumbe sita wakiwemo watatu kutoka Chama Cha Mapinduzi na watatu kutoka Chama Cha CUF, na kwamba wajumbe wa kamati hiyo wameonesha uzalendo wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maridhiano Mzee Hassan Nassor Moyo, amebainisha kuwa mambo yanayodaiwa kutolewa katika orodha ya Muungano sio mageni, kwani yalikuwemo kwenye mamlaka ya Zanzibar kabla ya kuungana na Tanganyika mwaka 1964.
No comments:
Post a Comment