TAMKO LA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI KUHUSIANA NA HABARI ILIYOCHAPISHWA NA GAZETI LA RAI KUHUSIANA NA KIFO CHA DKT. SENGONDO MVUNGI
Awali
ya yote Hospitali ya Taifa Muhimbili inapenda kutoa salamu za rambirambi
kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wa Dkt. Sengondo
Mvungi aliyefariki katika Hospitali ya Millpark, Johanesburg nchini
Afrika Kusini. Mwenyezi Mungu aiweke mahali pema peponi, roho ya
marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Amina.
Katika
gazeti la Rai Nguvu ya Hoja Toleo Na. 1092 la Jumatano Novemba 20, 2013
lilichapisha habari ukurasa wa tatu ikisomeka “Maisha ya Dkt. Mvungi
yangewezwa kuokolewa”
Gazeti
hilo lilidai kwamba baada ya marehemu Dkt. Mvungi kufikishwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili ilichukua zaidi ya saa sita kabla ya kupatiwa huduma
ya dharura aliyokuwa akihitaji na kwamba ni jambo la kawaida katika
Hospitali hii ya Taifa.
Tunapenda
kuwafahamisha umma wa Tanzania kuwa Idara ya Huduma za Dharura ya
Hospitali ya Taifa (EMD) imeimarika sana na huchukua takribani kati ya
dakika 30-45 tu kwa mgonjwa wa ajali kuhudumiwa na kupelekwa Taasisi ya
Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa matibabu zaidi. Na hivi ndivyo
ilivyokuwa kwa Marehemu Dr. Sengondo Mvungi.
Tunaomba
radhi kwa huduma ya kwanza ya CT Scan kutofanyika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kutokana na tatizo lililosababishwa na mawasiliano. Hata
hivyo, huduma ya CT Scan ya mara ya pili ilifanyika katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili na ilisaidia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha tiba
aliyokuwa anapatiwa na madaktari wa MOI.
Tunaendelea
kusisitiza kuwa uandishi wa habari za afya unahitaji kuzingatia maadili
ya sekta ya afya ili kutosababisha usumbufu usio wa lazima kwa
wananchi.
Ni
matumaini yetu kuwa Waandishi wa Habari watazingatia maadili ya kazi zao
kama tunavyoshauri mara kwa mara katika matoleo yanayohusu Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
Imetolewa na;
Ofisi ya Uhusiano
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Novemba 22, 2013
No comments:
Post a Comment