Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi,
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu
Zitto Zuberi Kabwe (pichani) ameanza ziara ya kikazi nchini Ujerumani
ambapo atahudhuria na kuhutubia Mkutano mkubwa wa masuala ya ushirikiano
wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Africa. Mkutano huo “Economic
Conference: Commitment to Africa Initiative” utafanyika Jijini Berlin
kuanzia tarehe 9 – 11 Desemba 2012 na umeandaliwa na Wizara ya
Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Serikali ya Ujerumani.
Katika ufunguzi wa Mkutano huo
ndugu Zitto atatoa mada kuhusu mgongano wa maslahi kati ya Kampuni
binafsi na Jamii ambapo ataongelea suala zima la makampuni makubwa ya
kimataifa yanavyonyonya rasilimali za Afrika bila kuwajibika kulipa kodi
na kuendeleza jamii zinazozunguka shughuli zao. Atazungumzia pia mitaji
kiduchu inayokuja Afrika na fedha nyingi inayotoroshwa Afrika kupitia
rushwa, ukwepaji kodi na wizi wa rasilimali. Afrika inapoteza zaidi ya
dola za kimarekani 583 bilioni kila mwaka kutokana na utoroshaji wa
fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa kwa kushirikiana na baadhi ya
viongozi wa Afrika. Hata hivyo Afrika inapokea takribani dola za
Kimarekani 80 bilioni tu kwa mwaka kutokana na Uwekezaji (FDI) na
Misaada (foreign Aid). Tanzania ni moja ya nchi inayopokea misaada mingi
kutoka nje na moja ya nchi ambayo rasilimali zake zinatoroshwa na
baadhi ya viongozi wake kutorosha fedha na kuzihifadhi kwenye mabenki ya
Ulaya kama Uswiss.
Mnamo tarehe 11 Desemba ndugu
Zitto atakuwa kwenye jukwaa moja na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani
kuzungumzia namna bora ya kushirikiana kati ya Ujerumani na nchi za
Kiafrika. Miongoni mwa mapendekezo ya Zitto ni kuondokana na mfumo wa
sasa wa ushirikiano wa misaada na badala yake kuwe na ushirikiano wa
kujengeana uwezo ili kila nchi iweze kuhimili maendeleo yake yenyewe.
Katika ziara hii Zitto atakutana
na Mawaziri Wakuu wa majimbo ya Nord Rhein Westphalen jimbo ambalo
limefanikiwa sana katika vita dhidi ya ukwepaji kodi unaotokana na raia
wa Ujerumani kuficha fedha kwenye mabenki ya Uswiss na wa jimbo la Lower
Saxony kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ukarabati wa Meli ya Liemba na
kujenga mahusiano kati ya Mkoa huu na Mkoa wa Kigoma pia kati ya mji wa
PapenBurg na Manispaa ya Kigoma.
Zitto anatarajiwa kutembelea
baadhi ya nchi nyingine za Ulaya na kukutana na watu mbalimbali katika
kuimarisha mtandao wa kimataifa dhidi ya utoroshaji wa fedha kutoka
Afrika (illicit money transfer). Pia atakutana na watu binafsi wenye
ujuzi na weledi katika masuala haya ya kupambana na watoroshaji wa
fedha. Zitto anataraji kurudi nchini mnamo tarehe 16 Desemba 2012. Kwa
namna itaakavyowezekana umma utapewa taarifa kuhusu ziara hii kupitia
akaunti ya twitter na facebook ya ndugu Zitto. Pia mada zote
atakazowasilisha zitawekwa kwenye blogu ya zittokabwe.com kila itakapowezekana.
Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu
Kiongozi wa Upinzani Bungeni anawatakia Watanzania wote kila la kheri
katika Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara. Utu, Uzalendo, Uadilifu na
Uwajibikaji ni silaha muhimu sana za kujenga Taifa lenye heshima na
jamii ya watu wenye fursa za kuendeleza maisha yao kwa haki na amani.
Tutimize wajibu wetu katika kuijenga Tanzania tuitakayo kwa ajili yetu
na kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa
Kigoma Kaskazini
8 Desemba 2012, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment