PINDA AWAZAWADIA WANAFUNZI 20 WALIOFANYA VIZURI MITIHANI YA KIDATO CHA SITA 2012
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda (kulia) akitoa pongezi kwa wanafunzi 20 waliofaulu
vizri katika mitihani ya kidato cha Sita 2012, bungeno mjini Dodoma.
Wanafunzi hao wakiwemo wasichana 10 na wavulana 10 wamepatiwa
vyeti,kuwazawadia kila mmoja kompyuta pakato Laptop na kila mmoja sh
laki mbili.
NA MAGRETH KINABO- MAELEZO, DODOMA
14/8/2012
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewataka wanafunzi
wote nchini kuwa na nidhamu , kujituma na kufuata maelekezo vizuri ya
walimu wao na kuepuka makundi mabaya ili kuweza kupata mafanikio
katika masomo yao.
Aidha Waziri Mkuu Pinda amewaasa wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu kidato cha sita wa mwaka huu kutumia uhuru vizuri watakaoupata kwenye maisha ya vyuo vya elimu ya juu bila kurudi nyuma katika maendeleo ya masomo yao.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Mkuu, Pinda Bungeni mjini Dodoma kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuwapongeza wanafunzi hao 19 kati 20 waliofanya vizuri katika mtihani huo,kutoka shule mbalimbali nchini, ambapo mmoja wao, Jamal Juma yuko nje ya nchi.
Wanafunzi hao ambao wote walipata ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani huo, saba kati yao wanatoka katika shule ya
wasichana ya Marian, watatu Mzumbe, wawili Fedha na wengine wawili
Kibaha. Waliobakia mmoja mmoja anatoka Kilakala, Ufundi Ifunda, Tabora
girls, Tabora boys, Minaki na Mpwapwa.
“Mmefanya vizuri. Mnastahili ! Hongereni Sana. Tunataka
ufaulu wenu uwe mzuri zaidi kwa vile sasa ninyi mnakweda kujenga
weledi. Mnakuwa wataalamu wa fani Fulani. Tumieni muda wenu kujifunza
zaidi kutafuta maarifa zaidi na kuvumbua mambo makubwa zaidi
yatakayowasaidia ninyi wenywe na jamii kwa ujumla kujiletea maendeleo,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Aliongeza kuwa ni vizuri utaratibu huo wa kuwatambua wanafunzi bora uwe endelevu na ikiwezekana
wapatiwe fursa ya kuendelezwa katika vyuo vikuu vya kipekee nje ya
nchi hususan kwenye fani zitakazojenga uwezo kwa taifa.
Waziri Mkuu alisema kati ya shule 10 ,ambazo wanafunzi hao wanatoka, wawili ni kutoka shule za kata, ambao ni Ester Marcel toka shule ya sekondari ya wasichana ya Olele Kilimanjaro na Brighton Lema toka shule ya sekondari ya Kitangiri, Mwanza.
“Napenda niwape pongezi za pekee wanafunzi hawa kwa jihudi kubwa walizozionesha. Kufaulu kwao kunadhihirisha kwamba shule hizi za kata tukiweka bidii kwa kuziwezesha zaidi zitafanya vizuri zaidi kama ilivyo katika shule nyingine,” alisisitiza .
Waziri
Mkuu pia aliwataka walimu wote nchini kushirikiana na wazazi na
serikali kwa pamoja kufundisha watoto kwa bidii ili waweze kufanya
vizuri katika masomo yao kama wanafunzi hao waliotunukiwa vyeti hivyo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi hao watazawadiwa pakato (laptop) na sh. 200,000, pia kila shule iliyotoa mwanafunzi bora itazawadiwa sh. milioni moja katika hafla maalum itakayofanyika jioni.
Wanafunzi hao wanatoka katika mchepuo wa PCM ambao ni 16 na mmojammoja toka mchepuo wa PGM, CBA, ECA na HKL.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri, Anna Makinda aliwataka wanafunzi hao kuwa makini na makundi kwa kuyasilikiza huku wakitumia akili zao huku akitoa changamoto shule nyingine kujitahidi kufanya vizuri.

No comments:
Post a Comment