HakiElimu waishauri Serikali, CWT kuhusu mgomo wa Walimu
Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kulia) akiwa na Meneja
wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda Shuli walipokuwa
wakitoa tamko la taasisi hiyo kuhusu mgomo wa walimu unaoendelea.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kulia) akitoa tamko kwa
wanahabari kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea nchini. Wa pili
kutoka kulia ni Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu.
Meneja
wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda Shuli (kushoto)
akijibu maswali anuai ya wanahabari katika mkutano huo.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
TAASISI
ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha Walimu
Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza
mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni
wanafunzi.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo
mbalimbali nchini.
Alisema
kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho
hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali
iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.
Mkurugenzi
huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi
na mazingira ya kazi ya watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa
watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza
mgogoro huo.
“HakiElimu
inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu
itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya
walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na
kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu
walio hoi,” alisema Missokia.
Aidha
amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku wakiendelea
kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na
Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu
inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza
wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii
bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi
na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si
wanafunzi,” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
“Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.
Pamoja
na hayo ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia
kati mgogoro huo na kutenga muda kujadili suala hilo kwa kina ikiwa ni
pamoja na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili
tatizo kama hili lisitokee tena.
“Bunge
lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji
na usimamizi wa elimu nchini. Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa
kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini
kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu
wa Bunge uko pale pale…” alisema Bi. Missokia.
Amekiri
kwamba ni kweli gharama za maisha zinazidi kupanda, huku mfumuko wa
bei nao unaendelea kuwaumiza watumishi kila siku, hivyo kuishauri
Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuweza kuwaboreshea
mapato watumishi wake.
“Serikali
ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si
kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma
watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na
maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.” Habari
hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment