|
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod
Slaa, amefufua upya sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, akitaka
serikali ithibitishe hadharani mtu anayetajwa kuhusika na tukio hilo.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika
mkutano wa hadhara mjini Ifakara, Morogoro jana, ikiwa ni sehemu ya
Operesheni Sangara awamu ya pili, Dk. Slaa aliyeambatana na viongozi
wakuu wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe,
alisema kuwa Serikali ya CCM imekuwa na kiburi cha kuwatisha wanaotaka
kutetea maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa imefikia hata hatua ya
wengine kutishiwa vifo, huku akitolea mfano wa kutekwa, kupigwa na
kisha kuumizwa Dk.Ulimboka,
aliyetendewa unyama huo usiku wa kuamkia Juni 26 katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Serikali ina nguvu ya kuvifungia vyombo
vya habari kwa sheria dhalimu ya magazeti ya mwaka 1977, lakini
haitaweza kuzuia midomo ya watu kujadili suala zima la kutekwa huko kwa
Dk. Ulimboka,” alisema.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akishangiliwa
kwa nguvu, aliongeza kuwa, kuanzia sasa CHADEMA itaanzisha mapambano
kwa ajili ya kutaka kupata ukweli juu ya aliyemteka Dk. Ulimboka.
Alisema kuwa miongoni mwa simu
zilizowasiliana na Dk. Ulimboka ni Ramadhan Ingondhur, aliyetajwa kama
mtu wa mwisho kabla ya kutekwa pamoja na namba ya Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mabwepande, aliyemtaja kwa jina la Abdallah Punja.
“Serikali na Usalama wa Taifa wanapaswa
kusimama hadharani na kuuambia umma Ramadhan ni nani na kwanini
anahusika na Idara ya Usalama wa Taifa.
“Mimi ni muumini wa Usalama wa Taifa na
wala siwaondolei hadhi, lakini kwa mwendo huu ni wao wenyewe ndio
wanajiondolea hadhi yao, na sasa wamekaa kufuatilia mikutano ya vyama
vya siasa, hususan CHADEMA,” alisema Dk Slaa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe
alisema umati uliokusanyika unaonesha namna wakazi wa Kilombero
walivyomthamini aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, marehemu Regia Mtema.
Mbowe aliomba jina la uwanja wa Ifakara
libadilishwe na kuitwa Uwanja wa Ukombozi, na kwamba hali hiyo iwe
chimbuko la ukombozi kwa Mkoa wa Morogoro.
Aliwataka wakazi wa Kilombero kuacha kulalamika na badala yake wachukue hatua kwa kuachana na CCM na kujinga na CHADEMA.
“Ndugu zangu kila mmoja ana wajibu wa
kujiuliza kafanya nini kwa ajili ya nchi yake, watoto wake na
anawaandalia nini siku zijazo. Tambueni tupo katika utwala usiowajali
na hili jukumu lenu ninyi wananchi kujiondoa katika hali hii na si kazi
ya Dk Slaa, Mbowe au Lissu,” alisema.
Mbali na Dk. Slaa na Mbowe, viongozi
wengine waliokuwa katika msafara huo ni Joshua Nassar (Arumeru
Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya
Mjini), Hamad Yusuph (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Suzan Kiwanga (Viti
Maalumu), Joyce Mukya (Viti Maalumu) na wengine wa makao makuu.
Naye Lissu, alisema baada ya kupita
kuanzia Mikumi hadi Ifakara, hajui ni kwanini bado wakazi wa wilaya
hiyo wanaendelea kuikumbatia CCM huku akishangazwa na kitendo cha
wananchi hao kuendelea kutozwa ushuru wa mazao ambao serikali
ilikwishaupiga marufuku.
Alisema ufike wakati wananchi wawakatae
viongozi wasiochaguliwa kuwa wawakilishi wao kwani wanasimamia masilahi
ya waliowateua kama inavyotokea sasa katika maeneo mbalimbali.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Mbilinyi alijibu
kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wapinzani wanapinga maendeleo,
akisema kwamba si kweli, kwani wao wanapingana na mipango inayowapa
fursa mafisadi kujineemesha, huku wananchi wakiendelea kuogelea katika
umasikini.
|
No comments:
Post a Comment