NDUGAI AWAGAWA WABUNGE WA CCM
Hatua
ya Naibu Spika, Job Ndugai, kukataa ombi la Mnadhimu Mkuu wa kambi
rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, kuwasilisha hoja ya kutaka ajali
ya MV Skagit, imekosolewa na kuwagawa wabunge kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Ndugai
akiongoza kikao cha Bunge juzi Ijumaa, alimzuia Lissu kuwasilisha hoja
ya kutaka kusitishwa hoja ya hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi
ya Wizara ya Chakula, Kilimo na ushirika, ili kufanyike mjadala kuhusu
ajali hiyo.
Naibu Spika huyo, alisema ingawa hoja ya Lissu ilikuwa nzito, lakini haikutolewa kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Hata
hivyo, Lissu alitoa taarifa akitetea kwamba alifuata utaratibu kwa
mujibu wa ibara ya kanuni ya 47 (3), ili apewe idhini na kiti cha Spika,
ndipo atoe hoja.
Lakini
Ndugai alisimamia katika uelewa na tafsiri yake kuwa Lissu alipaswa
kuzungumza baada ya kusimama kama ishara ya kutoa hoja, ili iungwe mkono
na wabunge wengine, lakini haikuwa hivyo.
Baadhi
ya wabunge kupitia CCM wameliambia NIPASHE Jumapili kuwa, hatua ya
Ndugai kuzuia hoja ya Lissu kwa kile kinachofananishwa ‘ubabe wa
kisiasa’, inakitia doa Chama Cha Mapinduzi.
Hata
hivyo, wabunge wengi hawataki kutajwa majina yao kwa kile wanachosema
kuepuka kuandamwa, kama ilivyotokea kwa Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo
Filikunjombe.
Filikunjombe
aliyeunga mkono hoja ya ajali ya MV Skagit kujadiliwa bungeni,
alifuatwa na baadhi ya mawaziri na kuulizwa kwa nini alifikia hatua hiyo
huku akijua hoja iliyotolewa ilitoka kwa wapinzani.
Mbunge
huyo kijana mwenye misimamo ya kuunga hoja zenye maslahi ya umma pasipo
kuathiriwa na itikadi za vyama, alisema ajali ya MV Skagit iliwaathiri
Watanzania bila kujali tofauti za itikadi zao.
Mbunge
wa Nzega (CCM), Hamis Kingwangalla, aliiambia NIPASHE Jumapili kuwa
ingawa Ndugai alitumia mamlaka ya Unaibu Spika, lakini alipaswa kutumia
busara zaidi kuhusu hoja ya Lissu.
“Hawa
jamaa (upinzani) hawakutaka kuahirishwa kikao ama mkutano wa bunge,
bali kujadili hoja ya ajali ya MV Skagit, kwa mtazamo wangu nadhani
angekubali hata kwa nusu saa, isingetuathiri,” alisema.
Mbunge
mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kukataa
kuijadili hoja iliyohusu maisha ya watu, iliifanya CCM ionekane haipo
kwa ajili ya wananchi wanyonge.
“Waliokufa
si wageni wale, ni raia wa Tanzania sasa kuikataa hoja ile, tena kwa
lugha ya mabavu ikichochewa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
haitoi taswira nzuri ya chama mbele ya umma,” alisema.
Hata
hivyo, Mbunge mmoja kutoka jimbo moja la mkoani Kagera ambaye hakutaka
pia jina lake litajwe gazetini, alisema hapakuwa na haja ya kuijadili
ajali hiyo kwa vile mamlaka nyingine zilikuwa zinaendelea kuifanyia
kazi.
“Binafsi
sijaona tatizo la Ndugai kuikataa hoja ya Lissu hata kama ingefuata
kanuni, kwa maana tayari kuna mamlaka nyingine zinalifanyia kazi,
hatuwezi kuwa taifa ambalo yakitokea majanga nchi nzima inaelekea huko,”
alisema.
Mbunge
huyo alisema, ndio maana licha ya kutokea ajali hiyo, taasisi nyingine
kama mashule, majeshi, wizara za serikali na nyinginezo hazikufungwa,
bali zilishiriki uzalishaji na utoaji huduma.
Kusitishwa
kwa Lissu kutoa hoja hiyo, kulisababisha baadhi ya wabunge wa upinzani
kutoka nje, kwa madai kuwa Bunge ‘linaburuzwa’ na serikali katika
kuwajibika kwa umma.
.jpg)
No comments:
Post a Comment