WAKATI
mjadala wa Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma ukitawaliwa na
vijembe, kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi, Mwenyekiti wa Taasisi ya
Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis Khalifa, amesema
mhimili huo wa dola umeoza na una udhaifu mkubwa unaotokana na kiti cha
Spika kukosa umakini na baadhi ya wabunge kukosa maadili wakati
wakijadili hoja zinazolihusu taifa.
Aidha sheikh huyo amelishambulia Bunge
baada ya juzi kushindwa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika kutokana na utoro uliosababisha kushindwa kufikia idadi ya
wabunge wanaopaswa kuwamo ukumbini wakati wa kupitisha bajeti kama
kanuni inavyoelekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Khalifa alisema mwenendo wa Bunge
hivi sasa unahuzunisha kutokana na tabia inayozidi kujengeka miongoni
mwao ya kutumia uhuru wao vibaya.
Bila kutaja majina, sheikh huyo maarufu
nchini alisema baadhi ya wabunge na hata viongozi wa mhimili huo
wanaenda kinyume na maadili ya Kitanzania kwa kukosa staha na kutoa
maneno ya dharau na kebehi hata matusi kwa wabunge wenzao.
“Wabunge wetu wakati mwingine
wanaonyesha kutojali heshima kwani utashuhudia kijana mdogo anashindwa
kuonyesha heshima kwa kiongozi wa serikali au mtu mzima anayelingana na
mzazi wake na wabunge au viongozi wazee nao wanakosa staha kwa mbunge
kijana na hivyo kulifanya Bunge lionekane kama kijiwe cha wahuni,”
alisema Khalifa.
Kwa mujibu wa Khalifa, vurugu ndani ya
Bunge zinatokana na wabunge wachache kutafuta umaarufu kwa njia ya
mkato kwa kutotii kanuni za Bunge na kwa kutumia lugha chafu.
“Wabunge wajue wananchi wanawaangalia.
Binafsi naona malumbano hayo ni jambo jema sana kwa sababu litawasaidia
wananchi kuwa makini kuchagua wabunge, hivyo mwaka 2015 tunategemea
wananchi watasahihisha makosa waliyofanya kuchagua baadhi ya wabunge
ambao tabia zao zinakera na hawafai kuendelea kubaki Bungeni,” alisema
Khalifa.
Hivi karibuni wakati wa mjadala wa
hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti
ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Mwenyekiti wa Bunge,
Steven Mabumba, alishindwa kuongoza kikao na kusababisha vijembe,
kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi.
Mvutano na malumbano hayo ya kisiasa vilimfanya Mbumba kuonyesha wazi upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani.
Mabumba alifikia hatua ya kutoa hata
kauli chafu Bungeni dhidi ya Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika,
akisema mbunge huyo “anawashwawashwa” na kutaka kusimama mara kwa mara
kuomba mwongozo.
Baadaye alimtoa nje Mbunge Kasulu Moses
Machali (NCCR Mageuzi) akidai kuingilia mjadala huo na kuongeza kuwa
alikuwa na ‘kiherehere’ cha kudandia mambo yasiyomhusu.
Malumbano hayo yaliyoendelea kwa siku
mbili, yalitokana na hoja ya mgomo wa madaktari na jaribio la kutaka
kuuawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka,
ambaye alitekwa nyara katika mazingira ambayo yanailazimisha serikali
kuendelea kujitetea kwamba haikuhusika kumteka daktari huyo.
Aliyeanza kuchafua hali ya hewa juzi
Bungeni ni Mbunge wa Viti Maalum na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella
Manyanya, ambaye alitoa tuhuma dhidi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), akisema kinahusika na mgomo wa madaktari na kwamba
waliomteka walivaa magwanda yanayoelekeana na nguo wanazovaa wafuasi na
wanachama wa CHADEMA.
Wakati Manyanya akiendelea kuzungumza,
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alisimama kupinga kauli hiyo
na kumtaka msemaji athibitishe au afute kauli yake.
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM)
Mwigulu Nchemba aliungana na Manyanya kwamba CHADEMA inahusika akitumia
kauli kama za Manyanya.
Hoja hiyo ilimtibua Mnyika, akatumia
kanuni mbalimbali kuwabana wasemaji (Manyanya na Mwigulu), na kuwataka
wathibitishe au wafute kauli zao.
Hata hivyo kauli ya Manyanya imewasikitisha baadhi ya wabunge wa CCM kwa madai kuwa mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alipotoka.
Hadi sasa Mnyika aliomba mwongozo wa
Spika kuhoji uhali wa Mwenyekiti wa Bunge, Mabumba, kutumia lugha ya
kuudhi kwa wabunge hao, lakini hadi sasa kiti cha Spika hakijatolea
uamuzi.
Malumbano mengine yaliibuka wiki
iliyopita baada ya baadhi ya wabunge kutaka kujadili chanzo cha ajali
ya meli ya MV. Skagit iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 150.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(CHADEMA), na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), walitaka Bunge
kujadili ajali ya meli hiyo kama dharura.
Mambo yalianza kwenda kombo baada ya
Lissu kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kifungu cha 47 (1)
kikiambatana na kifungu cha 47 (3) cha kutaka Bunge liahirishe shughuli
zake na kujadili jambo la dharura la taifa.
Katika mwongozo wake, Lissu alisema
katika kipindi cha maswali kulijitokeza swali linalohusu ajali za
baharini, ambapo wabunge wengi walionyesha hisia zao hasa kutokana na
ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea juzi na kuua Watanzania wengi.
“Mheshimiwa Naibu Spika huu ni muda
muafaka wa kulijadili suala hili hasa ikizingatiwa kuwa ni muda mfupi
tu tangu itokee ajali ya Spice Islander na kuua idadi kubwa ya
Watanzania inatokea tena ajali ya meli kuzama na kupoteza maisha ya
ndugu zetu, tujadili jambo hili kama dharura,” alisema.
Baada ya kauli ya Lissu, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi,
alisimama na kuliomba Bunge lisijadili jambo hilo kwa kuwa hivi sasa
taifa linashughulikia na uokoaji pamoja na kuhifadhi miili ya marehemu.
Baadaye alisimama mbunge wa Ludewa, Deo
Filikunjombe (CCM), akasema ipo haja kwa jambo hilo kujadiliwa bungeni
kama suala la dharura.
Alisema kuwa katika ajali nyingi
zilizotokea za meli ikiwemo ya Mv Bukoba na Mv Spice Islander kuliundwa
tume kuchunguza ajali hizo lakini matokeo yake hayakutolewa.
Mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali
(NCCR-Mageuzi), aliomba mwongozo na kuishutumu serikali kuwa imezoea
kutoa hoja kuwa jambo fulani linashughulikiwa na kusisitiza umuhimu
ajali hiyo kujadiliwa bungeni hapo kama dharura.
Akitoa mwongozo dhidi ya hoja ya Lissu,
Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, aliikataa hoja ya Lissu kwa madai hoja
yake haikuungwa mkono na wabunge licha ya kuitumia vizuri kanuni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick
Werema, aliingilia kati mabishano hayo na kufafanua kanuni hiyo kuwa
inazungumza wazi kwamba baada ya maswali mbunge ataomba mwongozo na
kutoa hoja ya Bunge kuahirishwa ili kujadili jambo la dharura kwa
taifa.
“Waheshimiwa wabunge kwa hili Lissu
alishatoa hoja, sisi binadamu tuna vichwa tuvitumie kufikiri na si
kufugia nywele tu,” alisema Werema jambo lililoibua tafrani ambapo
Lissu alidai ametukanwa na kutaka mwanasheria huyo afute kauli yake,”
Lissu na baadhi ya wabunge wa chama hicho waliondoka bungeni humo kwa hasira.
Ndugai naye wakati fulani aliwahi
kumkejeli Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), kwamba wananchi wa
jimbo hilo wamechagua kituko.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka amewataka
Watanzania kuwaombea viongozi wa ngazi zote wakiwemo wabunge ili wapate
hekima na busara kutoka kwa Mungu.
Akizungumza jana kwenye viwanja vya
Jagwani wakati wa maombi maalum kwa ajili ya taifa yaliyoandaliwa na
Chama cha Kitume cha Karismatiki Jimbo Kuu jijini Dar es Salaam
Tibaijuka alisema kuwa wabunge wanapaswa kisikilizana na kushindana kwa
nguvu ya hoja na si vinginevyo.
Tibaijuka pia aliwataka waumini hao
kuwaombea viongozi wa serikalini nao ili wapate hekima sawa na
aliyokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
“Waumini wa Karismatiki naomba tuliombee
Bunge, taifa na viongozi kwa ujumla kwani wakifuata nyayo za Baba wa
Taifa hakutakuwa na ufisadi wala migomo na mtu anayezungumzia udini,
itikadi za vyama au kubaguana huyo ana matatizo ya akili,” alisema
waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Mratibu wa Uinjilishaji Karismatiki
Arbogasti Kanuti alisema wanafanya maombezi ya mara kwa mara kwa kuwa
dini hutengeneza watu wenye maadili lakini wameamua kuliombea taifa kwa
sababu sasa linapitia changamoto nyingi ikiwemo rushwa, mauaji, migomo
na upatikanaji wa Katiba mpya.Chanzo. Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment