Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa mazingira litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) ofisini kwake leo alipokuwa akizungumzia zoezi la usafi na namna mkoa ulivyojipanga kutekeleza zoezi hilo siku ya 9 Disemba.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Kulia)
akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki
(Kushoto) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusu utekelezaji wa agizo la Mhe Rais la kufanya usafi wa mazingira
katika maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara.

Waandishi wa habari
wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es salaam juu ya usafi wa mazingira siku ya 9 Disemba.Picha zote na Raymond Mushumbusi – Maelezo
--
Na Lilian Lundo-MAELEZO
Mkuu wa Mkoa Dar es
Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa mazingira
litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9
Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata baada ya
kumalizika kwa maadhimisho hayo.
Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano. Mhe. Dkt John Pombe Joseph
Magufuli aliagiza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara
mwaka huu yatumike kwa kufanya usafi wa Mazingira kote nchini badala ya
kufanya sherehe za gwaride la askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Akiongea na vyombo vya
habari leo Mhe. Sadiki alianza kwa kumpongeza Mhe. Rais kwa uamuzi
aliouchukua wa kubadilisha sherehe za uhuru kuwa ni siku ya kufanya kazi
badala ya kwenda uwanjani na kuangalia gwaride na halaiki mbalimbali
kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
“Mhe. Rais katurejesha
kule tulipotoka ambako kauli mbiu ya sherehe za uhuru ilikuwa ni uhuru
na kazi au uhuru ni kazi wakati watanzania walikuwa wakiungana na
kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana,” alisema, Mhe. Sadiki.
Aidha, Mhe Sadiki
alisema, zoezi la usafi kwa mkoa wa Dar es Salaam litaanza rasmi
tarehe 1 Disemba mwaka huu na kumalizikia 9 Disemba mwaka huu siku ya
kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru na kuongeza kuwa zoezi hilo
litakuwa endelevu.
Mhe. Sadiki aliongeza kwa
kusema kuwa, uongozi wa mkoa umewaomba wadau kujitokeza kwa kuchangia
fedha au vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na amewataka
watendaji kushawishi wananchi wa maeneo yao kutafuta vifaa badala ya
kusubiri kuletewa na Halmashauri.
Pia, Mhe Sadiki
amewahimiza watendaji wa mitaa na kata kutimiza wajibu wao wa
kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi muda
wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko na pale inakapobainika eneo
fulani lipo katika mazingira ya uchafu basi mtendaji wa eneo hilo
atawajibishwa kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kosa la
kutotimiza wajibu wake.
Vilevile ametoa wito kwa
wananchi kuzingatia usafi kwa kuacha tabia za kutupa taka ovyo hasa
wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na kutokujisaidia katika mitaro au
vichaka ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira kunakopelekea kutokea
kwa magonjwa ya mlipuko .
No comments:
Post a Comment