TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA KUTOKWA DAMU MKOANI KIGOMA
JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
AFYA NA USTAWI WA JAMII

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA KUTOKWA DAMU MKOANI KIGOMA
Utangulizi
Ugonjwa wa Ebola
umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo hadi sasa nchi tatu
ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone,
zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya. Aidha, mpaka tarehe 19 Julai 2015,
idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 27,705 na vifo
11,269. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa
huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa udhibiti
wa ugonjwa huu wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.
Historia ya Mgonjwa
Mnamo tarehe 9 Agosti
2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni akiwa na dalili za
kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi, macho na
masikio. Vile vile alikuwa na dalili za kuchoka na mwili kuwasha.
Mgonjwa huyu
hakuwa na homa. Alipata matibabu katika hospital hiyo na kwa bahati mbaya mnamo
tarehe 10 Agosti, 2015 mgonjwa huyu alifariki dunia. Mgonjwa huyu alikuwa hana
historia ya kusafiri kutoka nje ya mkoa wa Kigoma wala kutembelewa na mtu
aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.
Mgonjwa huyu
alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika kambi ya
Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa mmojawapo wa wakimbizi
waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida chini ya Shirika la Kimataifa
linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9
Agosti 2015.
Hatua zilizochukuliwa
- Mgonjwa huyu alipatiwa matibabu katika hospitali ya Maweni Kigoma mpaka mauti ulipomkuta.
- Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu wa mgonjwa huyu, pamoja na wahudumu wa Afya waliomuhudumia mgonjwa huyu kuona kama wataonyesha dalili zinazofanana na ugonjwa aliokuwa nao mgonjwa huyu. Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu mwingine, aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
- Sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha ugonjwa huu.
- Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya uangalizi wa Afya mkoa, kwa kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za kuzuia maambukizi.
No comments:
Post a Comment