Benki ya Exim yachangia fedha Chuo Kikuu cha UDOM

Mkuu
wa Hazina wa Benki ya Exim, Bw. George Shumbusho (wapili kushoto)
akimkabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni kumi Makamu Mkuu wa
Chuo cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula (Kulia) ikiwa ni sehemu ya
mchango wa benki hiyo katika mfuko maalum wa chuo hicho maarufu kama
Endowment Fund, wakati wa hafla fupi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki. Akishuhudia ni Meneja Msaidizi wa Masoko wa Benki hiyo, Bi Anita
Goshashy
BENKI
ya Exim Tanzania imechangia fedha kiasi cha shilingi mil. 10/- kwenye
mfuko maalumu wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) maarufu kama “UDOM
Endowment Fund” ikiwa ni sehemu ya mpango wa benki hiyo kusaidia sekta
ya elimu nchini.
Mfuko
huo ulianzishwa na chuo hicho hivi karibuni kikilenga kuchangisha fedha
kwa ajili ya kusaidia baadhi ya mahitaji muhimu ya chuo sambamba na
uwekezeaji katika fursa za kitaaluma hususani kwenye masuala ya tafiti
za kisayansi.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki mara tu baada ya kupokea hundi
ya kiasi hicho cha pesa,Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof Idris Kikula
alisema kwa sasa pesa yote inayopatikana inahifadhiwa kwenye akaunti
maalumu ya uanzishwaji wa mfuko huo.
“Hadi
kufikia sasa tumefanikiwa kupokea takribani milioni 500/-ikiwa ni pesa
taslimu pamoja na ahadi kutoka kwa wachangiaji
mbalimbali.Tukishakamilisha mipango yote kuhusu aina za uwekezaji ndipo
tutajua kila uwekezaji utatengewa kiasi gani japo kwa kiasi kikubwa
pesa nyingi itaelekezwa kwenye miradi ya tafiti,’’ alisema.
Katika
kuthibitisha kuwa uwekezaji kwenye tafiti za kisayansi unaweza kuwa na
tija zaidi Prof Kikula alitolea mfano mafanikio ya hivi karibuni
waliyoyapata baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho ambao wameweza kubuni
program maalumu inayoweza kuendesha zoezi za chaguzi mbalimbali.
“Kwa
sasa programu hiyo bado inaendelea kufanyiwa majaribio na zaidi
tunarajia kuitumia kwenye chaguzi zetu za wanafunzi pale pale chuo,’’
alisema Prof. Kikula huku akitoa wito kwa taasisi nyingine za fedha
kuiga mfano wa benki ya Exim kwa kuchangia kwenye mfuko huo na maendeleo
ya elimu kwa ujumla.
Aidha,
Prof. Kikula alibainisha kuwa chuo hicho kitakuwa na wajibu wa
kuhakikisha kuwa kitaendelea kuwajulisha wachangiaji wote wa mfuko huo
kuhusiana na mwenendo mzima wa mfuko huo yakiwemo mafanikio yake.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Hazina wa benki ya Exim Bw. George
Shumbusho alisema benki yake iliamua kuunga mkono jitihada za chuo
hicho ikiwa ni namna ya kuthibitisha umakini wake kwenye masuala yote
yanayohusu sekta ya elimu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Exim
kamwe tusingeweza kuvumulia kuona kwamba kuna programu muhimu kama hii
inaendelea ndani ya taifa letu bila kutuhusisha kwa namna yoyote ile,’’
alisema Bw. Shumbusho huku akiahidi kwa niaba ya benki hiyo kuendelea
kuwezesha mfuko katika siku zijazo kulingana na matokeo na ufanisi wa
mfuko.
No comments:
Post a Comment