uzinduzi wa ushirika wa jitihada njema zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinbuzi Mhe. Ali
Mohamed Shein amesema kuanzishwa kwa vikundi vya ushirika (SACCOS) ni
njia moja ya kujiimarisha kiuchumi na kupambana na umasikini Visiwani
Zanzibar.
Ameyaeleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa Ushirika wa Jitihada Njema wa Bandari ya Zanzibar huko ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini
Zanzibar.
Amesema uanzishwaji wa vikundi vya ushirika hasa wa vijana na
kinamama, ni njia ya kuendesha maeneo maalumu ya kufanyia shughuli zao
za Biashara ndogondogo pamoja na kuzitambua rasilimali ambazo ziko
kwenye sekta zisizo rasmi vikiwemo vikundi hivyo.
Dr. Shein amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ya
awamu ya saba ambayo azma yao ni kuviimarisha vikundi vya ushirika
vinavyokwenda sambamba na ilani ya uchaguzi Mkuu ya Chama cha CCM ya
Mwaka 2010 ambalo amelibainisha wakati alipozinduwa Baraza la nne la
Wawakilishi tarehe 11 Novemba 2010 katika hutuba yake ya uzinduzi
huo.
Aidha ameeleza kuwa kufanya hivyo ni kuimarisha Mfuko wa Uwezeshaji wa
wananchi kiuchumi ili kukuza uwezo wa kutowa mikopo kwa wananchi na
kuwawezesha kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.
Hata hivyo amesema Serikali itashirikiana nao katika kuzitafutia
ufumbuzi changamoto zinazowakabili ili waweze kupata ufanisi zaidi wa
kuendeleza vikundi vyao.
Wakiwasilisha risala yao wana kikundi cha ushirika wa Jitihada Njema
wameliomba Shirika la Bandari la Zanzibar kuwapatia kiwanja ili waweze
kujenga ofisi yao kwa lengo la kukiendeleza kikundi chao.
Pia wamesema kwamba lengo la Ushirika wao ni kuwapatia mikopo
wananchi, kuutangaza ushirika wao ndani ya jamii ili kuwatengenezea
ajira vijana, kutatuwa changamoto zinazowakabili wanaushirika hao,
kusaidia kujuwa mbinu mbalimbali za elimu na kuwarahisishia
upatikanaji wa Bima ya Afya.
Hata hivyo wamesema tatizo kubwa kwa sasa linalowakabili katika
kikundi cha ushirika wao ni ukosefu wa ofisi yenye eneo la kutosha
kwa ajili ya shughuli zao jambo ambalo linawarejesha nyuma kwa kiasi
kikubwa katika utendaji wao kazi.
Ushirika huo ulianzishwa tarehe 31 Januari, 2004 ikiwa na wanachama
100 na hadi sasa una wanachama 200 na tayari wameshafunga mkataba wa
kupatiwa mikopo na Shirika la Bandari.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment