Header Ads

SIMBACHAWENE AIOMBA BENKI YA DUNIA KUISAIDIA TANESCO

00Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (mbele ) akiongoza kikao kilichokutanisha ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.
……………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameliomba Shirika la Fedha Duniani (WB) kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) ili liweze kuimarisha miradi ya usambazaji wa umeme nchini hususan vijijini.
Simbachawene aliyasema hayo wakati alipokutana na ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.
Alisema kuwa Tanesco inakabiliwa na changamoto ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya umeme hususan usambazaji wa umeme vijijini na kupelekea miradi mingi kutokamilika kwa wakati.
Akielezea maendeleo ya shirika hilo la umeme, Simbachawene alisema kuwa shirika hilo limeongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kubuni mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato hayo na kupunguza hasara zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Akielezea kuhusu upunguzaji wa bei ya umeme nchini, Simbachawene alisema kuwa Serikali imejenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam jambo litakalochangia upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika na kwa gharama nafuu ambalo ni moja ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
“ Ili kuhakikisha wananchi wananufaika na sekta mpya ya gesi, serikali ilibuni utaratibu wa kusomesha wataalam pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi katika vyuo vikuu vinavyotoa fani za mafuta na gesi ili kuwa na wataalamu watakaosimamia kwa ufanisi sekta ya gesi na mafuta.,” alisema Simbachawene .
Aliongeza kuwa mara baada ya kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya gesi na mafuta, serikali itaunda taasisi itakayokuwa na kazi ya kutoa ushauri katika masuala ya gesi na mafuta hususan wakati wa uingiaji wa mikataba.

No comments:

Powered by Blogger.