Header Ads

SERIKALI YAKUSANYA TAKRIBANI SHILINGI BILIONI 3 KUTOKANA NA KUONGEZEKA KWA MAKUSANYO YA MRAHABA WA MADINI


IMG_4403
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Bruno Mteta akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio yaliyopatikana baada ya ongezeko la makusanyo ya mrabaha kwenye madini ya ujenzi kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Kushoto ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Ukaguzi kutoka wakala huo Mhandisi Liberatus Chizuzu.


……………………………………………………………
Frank  Mvungi-Maelezo
SERIKALI imekusanya takribani shilingi bilioni 3 kutokana na  kuongezeka kwa makusanyo ya mrabaha uliotozwa katika madini ya Ujenzi katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani katika kipindi cha Juni mwaka 2011 hadi Novemba mwaka 2013.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Bruno Mteta wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Mteta alisema awali kabla wakala huo haujaanza ukaguzi wa madini ya ujenzi kiasi kilichokuwa kikikusanywa ni shilingi milioni tatu tu kwa mwaka hivyo kwa sasa kiwango hicho kimefikia wastani wa Bilioni moja kwa mwaka.
Alisema ukaguzi umeimarishwa katika vituo vyote ambavyo wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo wanalazimika kupita na kuonyesha vibali vya kusafirisha madini hayo ambavyo ni vocha maalum zinazotolewa na wakala huo ili kudhibiti wale wanaokwepa kulipa mrabaha.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa kila anayetakiwa kulipa mrabaha katika biashara ya madini ya ujenzi anafanya hivyo kwa kuimarisha ukaguzi kupitia vituo vyetu vya Afrikana,Pugu,Chalinze na katika maeneo yote yaliyobainishwa kutumika katika uchimbaji wa madini ya Ujenzi” alisema Mteta.
Katika hatua nyingine Mteta alisema kuwa ni wajibu wa kila mchimbaji na mfanyabiashara wa madini kulipa mrabaha unaostahiki ambapo kifungu cha 87 (6) cha sheria ya Madini ya mwaka 2010 kinachotaka mrabaha ulipwe kwa kuzingatia thamani halisi ya madini (gross value)yanapofikishwa sokoni au kwa mtumiaji.
Naye Mkurugenzi wa udhibiti na Ukaguzi wa Uzalishaji na Biashara ya Madini  Mhandisi Liberatus  Chizuzu alitoa wito kwa wananchi hasa wafanyabiashara wa madini ya ujenzi kuzingatia sheria na kanuni za Madini ili kulisaidia Taifa kujenga uchumi  imara.
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania TMAA kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki ulianzisha matumizi ya hati za mauzo ya Madini ya Ujenzi katika ukaguzi wa uzalishaji na mauzo ya madini ya ujenzi Kanda ya Mashariki (Mikoa ya Dar es salaam na Pwani) ambapo matumizi ya stakabadhi hizo yameongeza pato la Serikali kwa kiasi kikubwa kutokana na makusanyo ya mrabaha kwa kiasi kikubwa.

No comments:

Powered by Blogger.