ZANZIBAR NA OMAN KUSHIRIKIANA KIELIMU
Na Maua Ally .
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
imetaja majina ya wanafunzi saba wa Zanzibar
waliochaguliwa kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika fani mbali
mbali kupitia mpango wa masomo
unaodhaminiwa na Serikali ya Oman (OAF).
Akizungumza na waandishi wa habari
Ofisini kwake Mazizini baada ya kumaliza ziara ya siku nne nchini Oman, Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema wanafunzi hao
wamepatikana baada ya kuwafanyia mchujo
zaidi ya vijana 300 walioomba nafasi hizo.
Amesema kamati kutoka pande mbili, Zanzibar na Oman, ilikaa pamoja kupitia
majina ya wanafunzi wote walioomba na
kuchangua vijana saba waliofanya vizuri
zaidi katika mitihani yao na hivi sasa wanatafutiwa vyuo vya kusoma katika nchi
za Ulaya na Marekani .
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema vijana waliotakiwa kuomba nafasi hizo ni waliomaliza kidato cha
sita mwaka 2013 na kupata daraja la kwanza na la pili. Amewataja vijana hao kuwa ni Adam
Kassim Ali atakaesoma Uhandisi wa uchimbaji
mafuta, Al- Kassim Mohd Nassor El Mazrui atakaechuka fani ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano na Khadija Hilal
Al Habsy atakaesoma Sayansi na Hesabu.
Wengine ni Mize Burhan Omar na
Juwairia Mohd Ali ambao watasoma
Medicine, Ahmed Makame Mwadini na Salma Mohd Ali watakaochukua masomo ya ufamasia. Waziri Shamhuna amewapongeza
wanafunzi wote waliochaguliwa na kuongeza kuwa kuteuliwa kwao kunatokana na
uwezo uliotokana na matokeo mazuri ya mitihani yao.
Ametoa wito kwa wanafunzi wengine wa
kidato cha sita ambao watafanya mitihani yao mwaka huu wajitahidi kusoma kwa
juhudi na kufanya vizuri ili waweze na wao kuomba nafasi hizo za masomo na
hatimae kuchaguliwa.
Waziri wa Elimu amesema Serikali ya
Oman itaendelea kugharamia nafasi za masomo kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha
Taifa Zanzibar SUZA na wafanyakazi wengine ambapo watakaporejea watafanya kazi
SUZA.
“Nafasi hizo za masomo zitakuwa
katika vyuo vikuu mashuhuri Duniani ambavyo pia wanafunzi wa Oman
wanasoma,”alieleza Waziri Shamhuna.
Ameongeza kuwa tayari wazanzibari
watano wameshajiunga na vyuo vikuu kwa masomo ya shahada ya uzamili na uzamivu
na wengine sita wanakamilisha taratibu ili na wao waweze kujiunga mwaka huu.
Amesema kufuatia ziara hiyo, Serikali
ya Oman imekubali kuongeza nafasi zaidi kwa wanafunzi kutoka Zanzibar kusoma
katika Vyuo Vikuu vya Oman na kwa mwaka huu mwanafunzi Omar Juma Omar
ameshajiunga na Chuo Kikuu nchini Oman.
Aidha amesema wamekubaliana kuongeza
ushirikiano katika utoaji wa mafunzo kwa walimu wa masomo ya sayansi, Hesabati
na Kiingereza kwa Skuli za Sekondari na wahudumu wa maabara.
No comments:
Post a Comment