WAZIRI MKUU AINADI TANZANIA UGHAIBUNI
-Azialika kampuni za Kichina kuja kuwekeza Tanzania
WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda amewaeleza washiriki wa Maonesho 14 ya Kimataifa ya
China Magharibi kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya kwanza
katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na vituo vingi vya utalii na
akawataka waanze kumininika kwa wingi kuja nchini kutalii.
Ametoa
mwaliko huo leo asubuhi (Jumatano, Oktoba 23, 2013) wakati akihutubia
kwenye maonesho hayo ya kimataifa yanayojulikana kama 14th Western China
International Fair yaliyoanza leo jijini Chengdu kwenye jimbo la
Sichuan, China na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu ambaye
alikuwa miongoni mwa viongozi wa mataifa 11 waliopata fursa ya kuhutubia
maonesho hayo makubwa ya kimataifa, aliziomba kampuni za China kuja
nchini kuwekeza kwa kujenga viwanda vingi vya nguo zinazotokana na zao
la pamba.
Alitumia fursa hiyo pia
kuinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye ardhi kubwa tena yenye rutuba ambayo
inafaa kwa kilimo, na kuzisihi kampuni za Kichina ambazo zinataka
kuwekeza kwenye sekta ya kilimo zije nchini kwa ajili ya kulima kilimo
cha mashamba makubwa ya biashara.
Katika hotuba yake,
Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wawakilishi wa kampuni mbalimbali za
kimataifa zinazoshiriki kwenye maonyesho hayo kuwa, Tanzania ni miongoni
mwa nchi zinazolima pamba kwa wingi wakati China ni taifa ambalo
limebobea kwa viwanda.
“Sisi tuna pamba na
ninyi mna viwanda, nawaomba mje nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda
vya nguo kwani malighafi ipo ya kutosha,” alisema. Maonesho hayo
yanashirikisha kampuni 4,000 kutoka nchi 72 mbalimbali ulimwenguni na
majimbo mengine ya hapa China.
Ufunguzi wa maonesho
hayo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi saba, mawaziri wakuu wanne mbalimbali
akiwemo Pinda, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 25, wakuu wa
mashirika ya kimataifa wapatao tisa na mabalozi wanane wanaoziwakilisha
nchi zao hapa nchini China.
Gazeti la Serikali la
China Daily limeyaelezea maonesho hayo kuwa ni makubwa kufanyika katika
jimbo hilo na inatarajiwa kuwa mikataba yenye thamani ya dola za
Marekani bilioni 82 itasainiwa na kampuni mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu
utalii, Waziri mkuu pia alitumia fursa hiyo ya kuhutubia maonesho hayo
makubwa ya kimataifa kuinadi Tanzania katika sekta ya utalii na
kuwaeleza wafanyabiashara hao Tanzania ni nchi ya pekee katika ukanda wa
Afrika Mashariki yenye vivutio vingi vya utalii vikiwemo vitatu
vilivyoko kwenye maajabu saba ya Afrika.
“Kati ya maajabu saba
mapya ya asili barani Afrika, yaliyotangazwa Februari, mwaka huu,
maajabu matatu yako nchini mwetu ambayo ni mlima Kilimanjaro, hifadhi ya
Serengeti na Bonde la Ngorongoro,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na
vivutio hivyo lukuki lakini bado idadi ya watalii wanaofika nchini
kutoka China haijawa ya kuridhisha.
Alisema licha ya maajabu
hayo matatu, lakini pia kuna hifadhi nyingine za wanyama, hifadhi za
mambo ya kale na kisiwa maarufu cha Zanzibar. Alisema hata takwimu za
kimataifa zinaitaja Tanzania kama nchi ya pili duniani yenye vivutio
vingi kuliko nchi zingine ikiifuatia Brazil ambayo inaongoza kwa
vivutioa duniani.
“Pamoja na vivutio hivi
lakini idadi ya watalii kutoka China bado ni ndogo, sasa nawaambieni
njooni kwetu mjionee maajabu ya dunia,” alisema. Mkutano huo ulihutubiwa
na viongozi saba kutoka mataifa mbalimbali ambao wote walieleza
kunufaika na uhusiano wa kibiashara na China.
Viongozi hao ni magavana
wakuu ambao ni Quentin Bryce wa Australia na David Johnston wa Canada.
Wengine ni Rais wa Macedonia, Gjorge Ivanov, Waziri Mkuu wa Mongolia, N.
Altanhhuyag, Naibu Waziri Mkuu wa Berarus, Analy Tozik, Waziri Mkuu wa
zamani wa Ufaransa, Jean-Pierre Raffarin na Mwakilishi wa Umoja wa
Mataifa, Jan Mattassons.
Kwa upande wa Ardhi,
Waziri Mkuu alisema Tanzania bado ina ardhi kubwa ambayo haijaguswa kwa
kilimo, hivyo kampuni za China na zingine za mataifa mengine
yanayoshiriki kwenye maonesho hayo kuja kuwekeza nchini hasa katika
sekta ya kilimo.
Waziri Mkuu alisema,
anatoa ukaribisho kwa kampuni hizo kwa vile Tanzania sera yake ya
kibiashara ni ya kushirikiana na mataifa mengine na kukaribisha
wawekezaji wa nje na wa ndani kuja kuwekeza nchini katika maeneo ambayo
wanaona inafaa kufanya hivyo.
“Maonesho haya ni ishara
kwamba China inatoa fursa mbalimbali kwa watu wa ndani na nje ya nchi
kufanya biashara pamoja, na sisi tuna sera ya namna hii hivyo
tunawakaribisheni kuja nchini kuwekeza kwa wingi,” alisema Pinda.
Alisisitiza pia kuwa
wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta kama ya gesi ambayo
imegundulika hivi karibuni au kwenye makaa ya mawe na hata kwenye madini
ya chuma. “Ndiyo maana nasema kampuni za China njooni muwekeze kwetu
hasa katika sekta hizi.”
Waziri mkuu ambaye
alistaajabishwa na maonesho hayo ya kijimbo ambayo ni makubwa na yenye
mvuto kwa kampuni kubwa duniani, alitoa mwito kwa kampuni za China kuja
kushiriki kwenye maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya mwakani ambayo
yatafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 8, 2014.
Waziri mkuu jana ameondoka Chengdu na kueleka katika jimbo la Guangzhou ambako atamalizia ziara yake ya sikua tisa ya kikazi.
Katika ziara hiyo,
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji,
Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda;
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa
Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim.
Pia amefuatana na Balozi
wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo,
Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw.
Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega), Mkurugenzi wa Kituo
cha Uwekezaji, Bibi Julieth Kairuki na viongozi wa Tanzania Private
Sector Foundation, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfrey Simbeye.
HABARI NA PICHA KWA HISANI YA OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment