Ofisa wa JWTZ auawa vitani Kongo.
Msemaji wa JWTZ,Meja Erick Komba
Ofisa huyo aliyetambulika kwa jina la Luteni Rajabu Mlima, alifikwa na mauti alipokuwa anatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini humo kupitia kikosi cha Jeshi la Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini DRC (Monusco).
Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba, alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Luteni Mlima alipigwa risasi juzi wakati kikundi cha Tanzania kinakwenda kuwakinga raia wasidhurike na mapigano yaliyokuwa yanaendela kati ya Jeshi la Serikali ya DRC na Kikundi cha waasi cha M23 eneo la Kiwanja kwenye milima ya Gavana nchini DRC.
Meja Komba alisema kuwa taratibu za kuleta mwili wa marehemu huyo nchini zinafanywa na Monusco.
Aliongeza kuwa utaratibu wa kuupokea mwili huo, kuaga pamoja na mazishi zitatolewa baadaye na JWTZ.
Hadi sasa Tanzania imepoteza wanajeshi wake takribani 13, katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Agosti mwaka jana, Askari watatu wa JWTZ waliokuwa kwenye operesheni ya kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan (Unamid), walifariki kutokana na gari lao kusombwa na mafuriko.
Askari hao ni Sajenti Taji Chacha, Koplo Yusuph Said na Private Anthony Daniel.
Askari hao walifikwa na umauti wakati wakiwa kwenye doria ya kawaida kama moja ya majukumu yao wakati wakivuka mto Malawasha, katika kijiji cha Ahamada, baada ya gari lao la deraya kusombwa na maji.
Kadhalika, Julai 13, mwaka huu, askari saba wa JWTZ katika operesheni hiyo ya Unamid, waliuawa baada ya kuingia kwenye ‘ambush’ wakiwa katika msafara wa kuwasindikiza waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Askari hao walikuwa wakisafiri kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyala, na waliwekewa ‘ambush’kwenye eneo lililokuwa na mtelemko mkali na lenye utelezi, kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha.
Askari hao walishambuliwa kwa kushtukizwa na kusababisha kupoteza maisha yao.
Waliouawa ni Sajenti Shaibu Othman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Ally, Koplo Mohamed Chikilizo, Private Fortunatus Msofe, Private Rodney Ndunguru na Private Peter Werema.
Pia Agosti 28, mwaka huu Meja Mshindo akiwa na wenzake watano walishambuliwa na bomu nchini DRC na alipoteza maisha wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Private Hugo Munga alishambuliwa na bomu Agosti 28, mwaka huu na kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu na kufariki dunia Septemba 19, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment