Header Ads

NEWS ALERT: KAMANDA WA TRAFFIC MSTAAFU,SACP JAMES KOMBE AFARIKI DUNIA

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.

Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha usalama barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) mstaafu James Kombe amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kifo hicho Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema, Kombe alifariki Oktoba 22 mwaka huu na taratibu za mazishi zinaendelea.

Aidha Senso alisema Marehemu Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na Jeshi la Polisi tarehe 15 mwezi machi mwaka 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda ambapo alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.

Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni pamoja na Sagenti wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi(1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.

Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia katika Jeshi la Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na Kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha, Kigoma pamoja na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza ghasia Tanzania na hadi anastaafu alikuwa mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Tanzania.

No comments:

Powered by Blogger.