SIKU
moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki
kumtuhumu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO),
Dawal Nyenda, kusaidia majangili kutoroka nje ya nchi, jeshi la polisi
limech
ukua hatua ya kuunda timu kuchunguza tukio hilo.
Wakati hayo yakijiri, RCO Nyenda amesema
yote yanayotokea anamuachia Mungu, na kwamba hawezi kusema chochote kwa
sababu anamheshimu Kagasheki kama mkuu wake wa kazi.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera
Senso, alisema Mkuu wa jeshi hilo nchini, (IGP) Said Mwema, ameteua timu
maalum ya watu watakaokwenda jijini Arusha kuchunguza ili kupata
ukweli.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo,
walipata mshtuko kitu ambacho kilimfanya IGP Mwema kuchukua hatua hiyo
na kuahidi matokeo ya uchunguzi huo yatawekwa wazi ili kila mwananchi
afahamu.
"Jeshi la polisi linafanya kazi kwa sheria
na utaratibu, inapotokea mtumishi hasa kiongozi wa juu kutuhumiwa,
hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwamo kufanya uchunguzi kwa mujibu wa
sheria," alisema Senso.
Hata hivyo, Senso hakuwa tayari kutaja
timu hiyo ina watu wangapi na itachukua muda gani kukamilisha kazi,
badala yake alisema wananchi wanatakiwa kuliamini jeshi lao na majibu
yatapatikana haraka.
"Unajua kazi za jeshi ni vigumu kukupa
taarifa za kila kitu kinachofanyika, kitu muhimu hapa ni kwamba polisi
imeshtushwa na jambo hili na kazi hiyo itafanyika kwa uwazi mkubwa,"
aliongeza kusema.
Alisema timu hiyo itafanya kazi ya msingi
ya kusikiliza kila upande na endapo ikibainika kuna ukweli, taratibu za
kijeshi zitachukuliwa.
RCO 'NAMUACHIA MUNGU'
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani
Arusha, RCO Nyenda alisema mpaka sasa hajui kosa lake, hivyo yote
anamuachia Mungu ndiye anayejua ukweli wa jambo hilo.
Alisema yeye hajui chochote juu ya tuhuma
hizo kwani waziri hakumlalamikia wala kumtaarifu kama kuna jambo
limemkera yeye amelifanya.
"Mimi sijui chochote, taarifa zote
nimezisoma kwenye magazeti na kusikia kupitia runinga, muulizeni Kamanda
wa Mkoa kama yeye aliambiwa jambo hilo," alisema Nyenda.
Hata hivyo, alisema hawezi kujibizana na kiongozi huyo kwa sababu anamheshimu kama mkuu wake wa kazi.
WAZIRI NCHIMBI: "NIPO NJE"
Alipotafutwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kuzungumzia sakata hilo, alisema kupitia simu
yake ya mkononi kwamba hana taarifa kwa sababu yupo nje ya nchi kikazi.
"Ndugu mwandishi habari hii kwangu ni
mpya, nakuomba wasiliana na mtu niliyemuachia ofisi kwani kwa sasa nipo
nje ya nchi," alisema.
Juzi wakati akitangaza uwapo wa
`operesheni tokomeza majangili' nchini kote, Waziri Kagasheki alimtuhumu
RCO huyo wa Arusha kushiriki katika mchakato wa kuwatorosha raia wawili
wa Saud Arabia ambao walituhumiwa kwa ujangili.
Alisema, watu walikamatwa wakiwa na silaha na baadhi ya vithibitisho vinavyoonyesha walikuwa wakifanya kazi hiyo.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPIL
No comments:
Post a Comment