WEKUNDU wa Msimbazi, Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi
Kuu ya Bara, jana walifanikiwa kujiongezea pointi tatu katika kampeni
yao ya kutetea ubingwa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye
Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa.
Mechi hiyo iliyokuwa imegubikwa na kila aina ya ushindani kabla na
ndani ya dakika 90, bao pekee ambalo limeiwezesha Simba kufikisha pointi
15, lilifungwa kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 60.
Penalti hiyo ambayo ilikwamishwa wavuni na Rashid Gumbo na kumwacha
kipa Shaaban Kado akiwa hana la kufanya, ni baada ya Emmanuel Okwi
kuchezewa vibaya na Obadia Mwangusa, hivyo mwamuzi Alex Mahagi kutoka
Mwanza kuamuru penalti.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwani wakati Simba wakipambana
kutaka kuongeza bao, Mtibwa Sugar iliyo chini ya Kocha Mkenya Tom Olaba
ilicheza soka ya hali ya juu ikitaka kusawazisha bao hilo kama si
kuibuka na ushindi, lakini Simba walikuwa makini kuokoa hatari.
Kocha Olaba alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa Masoud Ally na Thomas
Mourice na kuwaingiza Omari Matuta na Zuberi Katwila huku Simba ikiwatoa
Jery Santo na Amri Kiemba wakiwapisha Juma Nyosso na Mussa Hassan
Mgosi.
Mabadiliko hayo ya pande zote hayakuweza kubadili sura ya mchezo kwani
licha ya kuwepo kwa mashambulizi makali kila upande, hadi filimbi ya
mwisho, Simba ndio walikuwa wababe kwa bao hilo moja.
Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 15 na kufanikiwa kupunguza
pengo la pointi kati yake na mtani wake Yanga yenye pointi 16 huku kila
moja ikiwa imecheza mechi sita tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti 21.
Katika mechi sita, Yanga imeshinda tano na kutoka sare moja huku Simba
ikishinda tano na kufungwa moja huku Mtibwa Sugar mabingwa wa ligi hiyo
mwaka 1999 na 2000, ikibaki na pointi tisa.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha wa Simba Mzambia Patrick Phiri
aliwapongeza vijana wake kwa kucheza kwa juhudi hadi kupata ushindi
kwani mechi ilikuwa ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao Mtibwa
Sugar.
Naye Olaba wa Mtibwa Sugar, amesema licha ya kufungwa, wachezaji wake
wanastahili pongezi kwa kiwango kizuri na kusema anaamini timu yake
itafanya vizuri katika mechi zijazo za ligi hiyo.
Katika hatua nyingine, mashabiki wa Simba waliokuwa wakisafiri kutoka
Dar es Salaam kwenda Morogoro kwa ajili ya mechi hiyo walipata ajali
wakiwa eneo la Mkuza, Kibaha, baada ya basi dogo walilokuwa wamepanda
kupinduka mara tatu wakati dereva akijaribu kukwepa gari jingine.
Hadi tunakwenda mitamboni, habari zilisema kuwa majeruhi wengi
waliokuwa wamepelekwa kwenye Hospitali ya Tumbi, Kibaha kwa matibabu
walikuwa wameruhusiwa isipokuwa watu watano.
Kutoka Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, timu ya Toto Africa
jana ilivuna pointi tatu baada ya kuwatandika vibonde wa ligi hiyo AFC
kwa bao 1-0, likifungwa dakika ya 68 na Jacob Massawe kutokana na pasi
ya Emmanuel Switta.
Naye Mwandishi Wetu, Safari Chuwa anaripoti kutoka Uwanja wa
Mkwakwani, mjini Tanga kuwa timu ya Azam FC ya Dar es Salaam ingawa
inautumia uwanja huo kama wa nyumbani, ilitoka sare ya bila kufungana na
maafande wa JKT Ruvu ya Pwani.
Licha ya timu hizo kushambuliana kwa nguvu, lakini zilijikuta zikimaliza dakika 90 bila kupata bao, hivyo kugawana pointi.
|
No comments:
Post a Comment