Watumishi wa umma kuweni karibu na wananchi, Balozi Mwinyi
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi akitoa mwongozo kwa wajumbe wa semina
ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoendelea kufanyika
kisiwani Pemba. Pamoja na mambo mengine amewahimiza wananchi
kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye mtangamano.
Mbunge wa jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akichangia jambo kwenye semina.
Sehemu ya wajumbe wakiendelea kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye semina.
Afisa
kutoka Ofisi za Uhamiaji Pemba Bw. Haji Kassim Haji akijibu hoja
mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wajumbe kwenye semina juu ya
upatikanaji wa Hati ya Kusafiria ya Afrika Mashariki.
Bw. Amedeusi Mzee akitoa mada kuhusu Soko la Pamoja na faida zinazopatikana kwenye soko hilo.
Luteni wa JKU naye akitolea ufafanuzi kwenye maswala mbalimbali yenayohusiana na maswala ya magendo.
Wajumbe
wakisikiliza kwa makini mada na majibu ya hoja mbalimbali walizokuwa
wakihitaji kufahamu kutoka kwa Bw. Amedeusi (hayupo pichani) na mjumbe
kutoka JKU.
Taasisi
za Serikali zimehimizwa ziwe karibu na wananchi ili ziweze kuwahudumia
na kuwaelimisha juu ya huduma inazozitoa. Wananchi wengi wamekuwa
wakilalamika mara kwa mara kuhusu watumishi wa umma kutotumia weledi na
ubunifu katika kuwahudumia wananchi jambo ambalo likiachwa liendelee,
Tanzania itaachwa nyuma ndani ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na ulimwengu mzima kwa ujumla.
Kauli
hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi katika semina
kuhusu elimu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake
inayotolewa na wataalamu wa Wizara yake kisiwani Pemba. Semina hiyo
iliyoanza jana inafanyika kwenye uwanja wa Gombani, Pemba na itamalizika
tarehe 18 Mei 2017.
"Kuna
fursa nyingi za kiuchumi katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki lakini kama wananchi wetu hatutawasaidia na kuwaelimisha
kuhusu nyaraka na masharti yanayokidhi vigezo wataachwa nyuma na kubaki
kuwa watazamaji na walalamikaji" Balozi Mwinyi alisema.
Wajasiriamali
walielezea masikitiko yao juu ya ugumu wa kupata hati za kusafiria
kutokana na mlolongo wa masharti hususan, inapotokea kuwa safari ni ya
ghafla. Aidha, wajasiriamali wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata tabu
kusajili bidhaa zao katika mamlaka zinazosimamia ubora wa viwango wa
bidhaa, chakula na madawa kwa kuelezwa kwamba bidhaa zao ni duni, hivyo
wameiomba Serikali iwawezeshe kupata teknolojia ya kisasa ikiwa ni
pamoja na vifungashio.
Balozi
Mwinyi alisisitiza umuhimu wa taasisi zote bila kukiuka Sheria, kanuni
na vigezo vilivyowekwa kurahisisha taratibu zao ili wananchi wapate
nyaraka zinazotakiwa kwa urahisi ili iwe wepesi kwao kuchangamkia fursa
za kiuchumi na kibiashara katika soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa hati za kusafiria, Afisa Uhamiaji, Bw.
Haji Kassim Haji alisema kuwa taratibu zilizowekwa hazina lengo la
kukwamisha shughuli ya mtu yeyote isipokuwa zimewekwa kwa kuzingatia
maslahi mapana ya nchi. Katika ulimwengu wa leo ambao unakabiliwa na
changamoto nyingi za kiusalama kama, ugaidi, uharamia, Biashara haramu
ya binadamu, uhamiaji haramu, lazima masharti yazingatiwe ili kuepuka
uwezekano wa kutokea uovu huo.
Aidha,
Balozi Mwinyi alishauri wajasiriamali wajiunge katika vikundi ili
masuala yao ikiwa ni pamoja na maombi ya hati za kusafiria yafanywe kwa
pamoja wakidhaminiwa na taasisi zinazosimamia shughuli zao.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Pemba, 16 Mei, 2017
No comments:
Post a Comment