MAAMUZI YA RUFAA ZA MAPINGAMIZI YA WAGOMBEA WA UBUNGE NA UDIWANI KATIKA UCHAGUZI MDOGO
Kwa mujibu wa
kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ilipokea
Rufaa moja ya kupinga Uteuzi wa Mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika
Uchaguzi Mdogo wa Bunge Jimbo la Dimani – Zanzibar.
Rufaa hiyo ilikatwa
na Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bwana
Juma Ali Juma akipinga Maamuzi ya
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani aliyemthibitisha Mgombea wa Chama Cha
Wananchi (CUF) Bwana Abdul Razak Khatib
Ramadhani kuwa ni mgombea halali.
Rufaa hiyo ilikuwa na sababu mbili ambazo ni:-
(i) Hakurudisha Fomu za Uteuzi kwa
mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea Ubunge. Katika kikao
chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016, Tume imepitia Rufaa hiyo na kuona sababu
zilizotolewa na mkata Rufaa hazina nguvu ya kisheria, kwa kuwa, Mgombea wa CUF
amerudisha Fomu za Uteuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Pia, Fomu zake za
Uteuzi zimesainiwa na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya Magharibi B. Kwa
mantiki hiyo, Tume imekubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la
Dimani – Zanzibar. Hivyo, Mgombea wa CUF
amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali na aendelee na kampeni za kugombea
nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.
Aidha, kwa mujibu wa
kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,
Tume imepokea Rufaa tatu; kutoka Kata ya Kijichi – Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha,
Mkoa wa Pwani na Kata ya Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Mkoa wa
Dodoma.
Kata
ya Misugusugu
Halmashauri ya Mji Kibaha, Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana
Gasper Melkiory Ndakidemi dhidi ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM
Bwana Bogasi Hussen Ramadhani.
Katika Kata ya
Kijichi, Rufaa ilikuwa ni ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas
dhidi ya mgombea wa CHADEMA Bwana Fredrick Felician Rugaimukamu.
Kata ya Ihumwa Rufaa
ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana
Magawa Edward Juma dhidi ya maamuzi
ya Msimamizi wa Uchaguzi.Tume katika kikao
chake cha leo tarehe 30 Desemba, 2016 imepitia Rufaa zote na imeamua ifuatavyo:
Rufaa ya mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi katika Kata ya Misugusugu Halmashauri ya
Mji Kibaha na ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah Shamas katika Kata ya
Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na
zimekataliwa. Hivyo, Tume inakubaliana
na Maamuzi ya Wasimamzi wa Uchaguzi wa Halmashauri hizo na wagombea waendelee
na Kampeni kwa mujibu wa Ratiba.
Kuhusu Rufaa ya Mgombea
wa CHADEMA kutoka Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tume, imepokea
barua ya Msimamizi wa Uchaguzi, Manispaa ya Dodoma, ikiwa imeambatishwa na barua
ya Mgombea wa CHADEMA kuiondoa Rufaa yake na kwamba anakubaliana na maamuzi ya
Msimamizi wa Uchaguzi ambayo yalimuengua. Pia, leo Tume imepokea barua za
kujitoa Ugombea za wagombea wa CHADEMA na ACT - WAZALENDO katika Kata ya
Ihumwa. Kwa maana hiyo Rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa CHADEMA Kata ya
Ihumwa imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa na amejitoa ugombea kabla
haijasikilizwa.
Mwisho,
Tume inavisisitiza Vyama vya Siasa, Wagombea na Wananchi wote wa maeneo yenye
Uchaguzi Mdogo kufanya Kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Maadili ya Uchaguzi.
Imetolewa na:-
Jaji Mkuu (Mst.
Znz) Hamid M. Hamid
MAKAMU MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA
UCHAGUZI
30/12/2016
No comments:
Post a Comment