Header Ads

CHUO CHA ARDHI CHATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI 104 WALIOFAULU

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Idrissa Mshoro (katikati kulia) akiteta jambo na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga(katikati kushoto), pembeni kulia ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho (Mipango, Fedha na Utawala),Prof. Robert Kiunsi, pembeni kushoto ni Maafisa Waandamizi wa chuo hicho. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Idrissa Mshoro akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa chuo na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma wakati wa shughuli za ugawaji wa vyeti na zawadi kwa wanafunzi waliofaulu masomo mbalimbali uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Mmoja kati ya washindi wa jumla wenye alama za juu, Anyighwile Lwijiso akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wafadhili ambao ni Kampuni ya Hightech System mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo Kikuu cha Ardhi kimetoa zawadi na tuzo kwa wanafunzi 104 waliofanya vizuri kitaaluma ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wengine kuweka juhudi katika masomo.
Zawadi hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ambaye ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi wanne kati ya waliofanya vizuri wamepata alama sawa hivyo kuibuka washindi wa jumla kwa mwaka 2016. 
Akisoma hotuba wakati wa sherehe hizo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga amesema kuwa sherehe hizo zimekuwa zikiwezeshwa na wadau mbalimbali waliojitoa kwa hali na mali kutoa zawadi na tuzo kwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye vipengele mbalimbali vya taaluma hivyo amewasihi wadau hao kuendelee kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wanafunzi hao ili kuwashawishi wanafunzi wengine kufanya vizuri.
“Zawadi mbalimbali zinazotolewa na wafadhili zimekua zikiwasaidia wanafunzi hawa kuongeza tija kwenye maisha yao ya kielimu na kiuchumi kwani wengi wao wamekuwa wakizitumia fedha hizo kama mitaji ya kufanyia biashara pindi wamalizapo masomo yao,”alisema Prof. Kassenga.
Amefafanua kuwa mwaka huu umekuwa wa tofauti kwani idadi ya wanafunzi wanawake na wanaume waliopata tuzo hizo iko sawa tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo wanawake walikua wakiongoza kwa asilimia 3.7 kwa kupata tuzo nyingi wakati wanaume wakiwa ni asilimia 2.2. 
Prof. Kassenga ametaja baadhi ya zawadi zilizotolewa na wafadhili walioshiriki katika shughuli hiyo kuwa ni vyeti, Kompyuta mpakato (laptop),vifaa vinavyotumika katika kupimaji wa ardhi pamoja na fedha taslimu.Aidha, Prof. Kassenga ametoa rai kwa kwa wanafunzi wote waliomaliza chuoni hapo kuwa juhudi walizokuwa wakizionyesha wakati wa masomo waende wakaziendeleze katika jamii zinazowazunguka pamoja na kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa ili wakawe mfano bora kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Emily Elandogo ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliopewa zawadi hizo amewashukuru walimu wa chuo hicho kwa elimu wanayoitoa ambayo itakua ni chanzo cha kuwaletea maendeleo sehemu yoyote watakapokuwa pia ametoa ushauri kwa wanafunzi wenzake kuitumia vizuri elimu waliyoipata ili iweze kuwasaidia katika maisha yao. 
Mahafali ya Kumi ya chuo hicho yanategemewa kufanyika Disemba 3 mwaka huu katika viwanja va chuo hicho ambapo wahitimu wa shahada mbalimbali watatunukiwa stahili pamoja na vyeti vyao.

No comments:

Powered by Blogger.