TFF YA MALINZI YAMLILIA SHEIKH SAID MOHAMMED WA AZAM
MZEE SAID WAKATI WA UHAI WAKE, AKIZUNGUMZA MBELE YA RAIS WA AWAMU YA NNE, JAKAYA MRISHO KIKWETE |
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia leo Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Taarifa
za kufariki dunia kwa Mzee Said Muhammad ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi zimethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC,
Saad Kawemba aliyesema kwamba alifariki dunia katika wodi ya Wagonjwa
mahututi (ICU) hospitalini hapo baada ya kuzidiwa ghafla nyumbani kwake.
Kutokana
na kifo hicho, Rais wa TFF Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Yahya Mohammed, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya
Ligi, Boniface Wambura, Uongozi wa Klabu ya Azam, familia ya marehemu,
ndugu, jamaa na marafiki. Amewataka kuwa watulivu wakati huu mgumu wa
kumpoteza Mzee Said Muhammad.
Katika
salamu zake, Malinzi amemwelezea marehemu Said Muhammad kuwa alikuwa
hazina katika mpira wa miguu nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa
kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF.
Aliongoza
Klabu ya Azam kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo
ianzishwe.
“Ndani
ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Mzee Muhammad ndiye aliyekuwa na umri
mkubwa ukilinganisha na wajumbe wengine, lakini alikuwa hakosi vikao
muhimu. Mchango wake wa mawazo ulikuwa nguzo kwetu. Nimepokea taarifa
hizi za kifo chake kwa masikitiko makubwa,” amesema Rais Malinzi leo
mara baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.
Taratibu
za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu. Sheikh Said Muhammad
atazikwa kesho Jumanne alasiri katika makaburi ya Kisutu baada ya mwili
wake kuswaliwa msikiti wa Maamur ulioko Upanga, jijini Dar es Salaam.
Inna lillah wainn ilayh Rajiuun.
No comments:
Post a Comment