LHRC YATOA TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA WAZEE DUNIANI
Dkt.Helen Kijo-Bisimba |
OKTOBA
Mosi (1) ya kila mwaka ni siku iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa
kuadhimisha uwepo wa wazee katika jamii kote ulimwenguni. Siku hii
ilianza kuadhimishwa rasmi Oktoba 1, 1991 kwa lengo la kuongeza uelewa
kuhusu mambo yanayowalenga wazee ikiwemo kutoheshimu haki za wazee,
kutazama mahitaji na maslahi ya wazee na kuhakikisha mzee popote alipo
ulimwenguni anapata huduma za msingi za kijamii kama vile huduma bora za
afya na matibabu.
Mahususi, siku hii imekuwa na lengo la kuutambua mchango wa wazee katika jamii kwa wakati husika na wakati uliopita katika mataifa yao. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunatumia fursa hii kuwapongeza wazee wote duniani na hususan wazee wa Tanzania.
Pia tunatumia siku hii kuikumbusha serikali na mihimili mingine ya dola pamoja na wanachi wote kwa ujumla kuheshimu wazee wetu kama hazina ya taifa. Pia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitumia siku hii kuungana pamoja na wazee wanaodai haki yao kwa zaidi ya miaka 20.
Mathalani, wazee waliotumikia iliyokuwa jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya kuvunjika kwake mwaka, 1977 ambao mpaka leo wameendelea kupambana na kudai haki yao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pia tunaitumia siku ya leo kuitaka serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania kutoa msimamo wake juu ya kesi ya madai ya waliokuwa walinzi wa ubalozi wa marekani nchini Tanzania wakijulikana kama 'mission security force' katika Ubalozi wa Amerika kwa serikali ya Amerika – 1984.
Sambamba na hayo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakemea vikali vitendo vya mauji ya wazee kwa imani za kishirikina vinavyozidi kupamba moto nchini, watoa huduma wa afya wanaotumia lugha za kuudhi dhidi ya wazee, vijana wanaorubuni wazee kuuza mali zao na kuwatapeli hususani ardhi kuacha vitendo hivi ili kuheshimu tunu hii adhimu ya taifa..
Tunaungana na jamii ya ulimwengu kusimama kupinga mitazamo hasi juu ya wazee na uzee kiujumla.
Wazee ni hazina kwa Taifa tuilinde hazina hii kwa uendelvu wa jamii yetu.Tuwatunze na kuwasikiliza wazee wetu.
Imetolewa jana Tarehe 1/10/2016
Dkt.Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
No comments:
Post a Comment