WAZIRI MKUU AWAWEKA SAWA WATUMISHI WA OFISI YAKE
*Asema safari imeiva,
ataka wajipange kuhamia Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema safari ya kuhamia
Dodoma imeiva na amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wajipange
kisaikolojia.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Agosti 18, 2016) alipokutana
na kuzungumza na watumishi wa ofisi yake kutoka taasisi, idara na vitengo
mbalimbali waliopo Dar es Salaam.
Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao watambue kuwa
uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973
kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu wakati huo kumekuwa na juhudi mbalimbali
zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa
kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa
kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa
CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa
na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.
“Napenda kuwatoa hofu, mambo yanaenda vizuri ila
mtambue kuwa safari imeiva sasa. Kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama
ambavyo imepangwa,” alisema.
Aliwataka watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni
mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu
na uaminifu. “Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana
tuliyonayo. Tufanye kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika
kwa ufanisi na kinafanikiwa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18,
2016.
No comments:
Post a Comment