WALIOFICHA SUKARI WAASWA KUIFICHUA MARA MOJA.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka
wafanyabiashara wote walioficha sukari katika maghala yao, kuanza
kuisambaza mara moja, vinginevyo serikali itachukua hatua kali ikiwa ni
pamoja na kuinyang'anya sukari hiyo na kuisambaza kwa wananchi bure.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 06 Mei, 2016 katika mikoa ya
Singida na Manyara wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti
waliosimamisha msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kwenda Arusha.
Dkt.
Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwafuatilia wafanyabiashara
wanaofanya njama za kuficha sukari na kusababisha upungufu wa bidhaa
hiyo, na ameapa kuwa serikali yake itawachukulia hatua kali
watakaobainika kufanya hivyo.
Pamoja
na kutoa maagizo hayo Rais Magufuli amewaondoa shaka watanzania juu ya
upungufu wa sukari, kuwa serikali imeagiza sukari kutoka nje ya nchi
ambayo itasambazwa kwa wananchi kwa bei nafuu ili kufidia upungufu
uliopo.
"Wale
wote waliokuwa wameficha sukari waiachie, wasipoiachia sukari, huwezi
kuificha kama sindano, nimeshaagiza vyombo vya dola, vikague magodown
yote, atakayekutwa na sukari ameificha, yule ni mhujumu uchumi kama
wahujumu wengine, asije akanilaumu, asijee-akanilaumu, na ninasema kwa
dhati, wewe mfanyabiashara uliyepata nafasi ya Tanzania kuleta bidha za
sukari, halafu
unanunua unakwenda kuficha ili kusudi wazee hawa wahangaike, ili mwezi
mtukufu wa Ramadhani utakapoingia watu wakose sukari, dawa yao ninayo"
Amesema Rais Magufuli.
Aidha,
akizungumza katika miji ya Katesh, Babati, Dareda na Magugu Mkoani
Manyara Dkt. Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kukosa
maeneo ya kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji, na amemuagiza Mkuu wa
Mkoa wa Manyara Bw. Joel Bendera na wakuu wilaya za mkoa huo
kukamilisha mchakato wa kuyapitia mashamba yote yaliyotelekezwa na
wamiliki wake, kisha wawasilishe taarifa kwake ili afute hati za umiliki
wa mashamba hayo na kuamuru wagawiwe wananchi.
"Kero
kubwa katika maeneo haya, pamekuwa na mashamba makubwa ambayo
yalichukuliwa na wenye pesa, halafu yale mashamba hawayaendelezi, na
wanapoacha kuyaendeleza wanawachukua wananchi masikini na kuanza
kuwakodisha, kwa kukusanya fedha, mniachie hili ndugu zangu
nitalishughulikia" Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Mjini
Babati Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi waliodai kudhulumiwa
haki zao na kujikuta wakipoteza mali ikiwemo nyumba za kuishi na mazao
na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupanga siku za kusikiliza kero za
wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Rais
Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Dodoma kwa njia ya barabara na
kesho anatarajia kutunuku kamisheni kwa maafisa wapya wa Jeshi la
wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 katika chuo cha mafunzo ya jeshi
Monduli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
06 Mei, 2016.
No comments:
Post a Comment