Header Ads

Msama: Waziri Nape ni faraja Tamasha la Pasaka

MWENYEKITI wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama amekoshwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Pasaka litakalofanyika Mwanza Machi 27 na kueleza kwamba ni faraja kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema Nape ni mmoja wa walezi wa tamasha hilo ambalo mwaka huu linatarajia kuanzia Geita Machi 26 na kumalizikia Kahama Machi 28.

“Maandalizi kuelekea Tamasha la Pasaka yanaendelea vema na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri Nape, hivyo wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wajiandae kupokea ujumbe wa neno la Mungu kupitia viongozi wa dini na waimbaji wa muziki wa Injili,” alisema Msama  na kuongeza.

“Tunafurahishwa na Waziri Nape kukubali kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka, kwa sababu ni mmoja wa wanaoweza kusaidia mipangilio ya Matamasha yanayoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions kama ilivyokuwa Tamasha la Krismasi lililofanyika mwaka jana,” alisema Msama.  
  
Aidha Msama anatumia fursa hiyo kuwaweka bayana waimbaji waliothibitisha kushiriki  Tamasha la Pasaka ambao ni pamoja na Rose Muhando, Bonny Mwaitege, Upendo Nkone, Jesca BM Honore, Christopher Mwahangila, Joshua Mlelwa, Sifael Mwabuka, Jenipher Mgendi, Kwaya ya AIC Makongoro ya Mwanza na Kwaya ya Wakorintho wa pili kutoka Njombe.

Anavitaja viingilio katika tamasha hilo litakalofanyika mikoa ya Kanda ya Ziwa ni Sh. 5,000 kwa wakubwa na kwa watoto Sh 2,000. Msama alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vema na kutoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi.

No comments:

Powered by Blogger.