JESHI LA POLISI LAJIPANGA KUFANYA KAZI KWA UBORA ZAIDI
Na. Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.
Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki amewataka askari polisi
kote nchini kufanya kazi kwa weledi ili kuendana na kasi ya serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na rais Mhe.John Pombe Magufuli ambayo lengo
lake ni kuwatumikia wananchi.
Hayo
aliyasema wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano kwa askari
polisi watakaokuwa wakitoa huduma katika vituo vya kuhamishika (mobile
police station) vinavyotarajiwa kuanza kazi katika mkoa wa kipolisi
Kinondoni (mkoa wa mfano) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa kuboresha
usalama wa raia na mali zao nchini, mpango ambao unatekelezwa na Jeshi
la Polisi kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais, Usimamizi na utekelezaji wa
miradi (PDB).
Alisema
katika kipindi hiki kila askari anatakiwa kufanya kazi kwa kasi na
kufuata maadili ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora
kwakuwa ndio lengo la Jeshi la Polisi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa
vyema na kwa wakati katika vituo vya Polisi kwakufuata taratibu na
misingi ya kazi za Polisi.
Aidha,
aliwataka askari hao ambao watakuwa wakitoa huduma katika vituo hivyo
vya kuhamishika kuhakikisha kuwa lengo la kuwepo kwa vituo hivyo
linatimia kwa kutoa huduma bora na ya haraka ili kujibu yale yote
yaliyoainishwa katika mpango huo.
“Jambo
kubwa lililoainishwa katika maabara iliyoandaa mpango huu ni suala la
kuchelewa kufika katika matukio ya kiuhalifu hivyo kwa kutumia raslimali
zilizopo pamoja na vituo hivi vya kuhamishika ni wazi kuwa sasa
tutajitahidi kufika katika matukio mapema”Alisema Kaniki.
Kwa
upande wake mkuu wa kitengo cha kusimamia mpango huo ndani ya Jeshi la
Polisi, Naibu kamishna wa Polisi DCP Goodluck Mongi alisema, lengo la
mafunzo hayo ya siku tano ni kuwapa utayari askari katika kutekeleza
majukumu yao ili kuleta matokeo makubwa katika mkoa wa kipolisi
Kinondoni ambao ni mkoa wa majaribio wa mpango huo ndani ya Jeshi la
Polisi.
Alisema
mpango huo umeainisha mambo mengi ikiwemo kuwepo kwa vituo vya
kuhamishika ili kuweza kuwafikia wananchi kwa haraka na vituo hivyo
vitawekwa kwa awamu ili kuhakikisha kila anayehitaji huduma za Kipolisi
hapati shida kwa kwenda umbali mrefu kuzitafuta hali itakayopelekea
kudhibiti na kuzuia uhalifu wa aina zote.
No comments:
Post a Comment