WAZIRI MKUU MAJALIWA: TUJIKITE KUIMARISHA MIUNDOMBINU YETU ILI TUKUZE UCHUMI
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua mkutano wa miradi ya ubia katika ujenzi
wa Miundombinu kati ya Japan na Tanzania kwenye hoteli ya Hyatt
Regency- Kilimanjaro jijini Dar es salaam Januari 14,2016.
………………………………
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amewataka watanzania kujikita katika kuimarisha miundombinu ili kukuza
uchumi, kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa
shughuli mbalimbali mfano kilimo na biashara.
Akizungumza na wadau wakati
akifungua mkutano wa Miradi ya Ubia katika Ujenzi wa Miundombinu kati
ya Tanzania na Japan(TANZANIA -JAPAN PUBLIC -PRIVATE QUALITY
INFRASTRURE CONFERENCE) uliofanyika leo, katika hoteli ya Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam, amesema sekta binafsi inasaidia katika ujenzi
wa miundombinu na sekta ya usafirishaji kwa ujumla, ambapo ni muhimu
kwa vile inasaidia kuboresha maisha ya watu.
“Serikali kupitia Kituo cha
uwekezaji nchini (TIC) imeandaa mazingira mazuri ya biashara inayosaidia
wawekezaji kuja kuwekeza nchi, matumaini yetu ni kwamba kutokana na mkutano huu wawekezaji wa ndani mtapata fursa ya kujifunza na kujiunga katika kampuni ambazo zitawasaidia kushirikiana na kampuni za kijapani na kuweza kupata ujuzi, utaalamu wa kiutawala na uwezo wa kuwa wabunifu zaidi hasa katika masuala ya miundombinu.” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea
kwa kusema mkutano huu utaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na
Japani, na kutoa fursa ya kubadilishana ujuzi kwa wakandarasi, washauri,
kampuni za biashara na uhandisi kutoka Japani na Tanzania, vilevile
utawawezesha kujenga mtandao kwa kushirikiana na makampuni ya nchi hizi
mbili.
Kwa upande wa miundombinu na
usafirishaji, Tanzania ina ukubwa wa barabara zinazofikia kilomita
87,581, kutokana na sera na jitihada mbalimbali kwa kipindi cha miaka
10 (2005-2015) jumla ya kilomita 17,762 zimefikia hatua mbalimbali za
ujenzi.
Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema,
Tanzania ina mifumo miwili ya reli, reli ya kati yenye kilomita 2,706
na reli ya ‘Tanzania Zambia Railway Authority’ (TAZARA) yenye kilomita
975. Pia, ina Bandari kuu za Dar es salaam, Tanga na Mtwara .
Kwa upande wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA), kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa
(National ICT Broadband Backbone -NICTBB) kwa kutumia mfumo wa baharini
(SEACOM, July 2009) na (EASSY April,2010) tayari nchi jirani za
Rwanda, Zambia na Kenya zimeunganishwa na mkongo huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani, amesema
miundombinu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yeyote ile
duniani. Tanzania na Japani zimeshirikiana katika ujenzi na uboreshaji
wa miundombinu mbalimbali, mfano barabara za Dodoma –Iringa, Namtumbo
–Tunduru, Dodoma – Babati inayoendelea kujengwa, upanuzi wa barabara
ya Gerezani pamoja na ‘fly over’ ya TAZARA.
Naye, Waziri wa Ardhi,
Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Takatoshi Nishiwake amesema,
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipotembelelea Japani alisema
angependa kuona Japani na Tanzania zinashirikiana katika masuala ya
ujenzi wa miundombinu.
Ameendelea kwa kusema kuwa,
Serikali ya Japani inapenda kubadilishana ujuzi na Tanzania katika
masuala ya miundombinu, pia ni matumaini yake kuwa washiriki kutoka
pande zote mbili wanapata fursa ya kubadilishana ujuzi na kujifunza
zaidi. Vile vile kupitia mkutano huu mahusiano ya nchi hizi mbili
yataimarika zaidi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, JANUARI 14, 2016
No comments:
Post a Comment