WACHUUZI WA TANZANITE WALIA NA LESENI
Na Woinde Shizza.
WACHUUZI wa
madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
wameiomba Serikali kutowabana walipe leseni ya ununuzi, kwani uwezo wao ni
mdogo na wao ni madalali siyo wanunuzi wa madini hayo.
Wakizungumza juzi wachuuzi
hao walidai kuwa hawapingi kulipa mapato ya serikali ila zoezi la ulipaji wa
leseni ya kununulia madini ya Tanzanite ingetakiwa kutekelezwa kwa
wafanyabiashara peke yao na siyo kwa wachuuzi wadogo.
Mmoja kati ya
wachuuzi hao Anturusia Chande alisema wengi wao wanapewa madini hayo na
kuzunguka kwenye masoko ya Mirerani kwa lengo la kujikimu maisha yao ikiwemo
kusomesha watoto, mavazi, chakula na matibabu.
“Sisi hatuvuki na
madini nje ya eneo la Mirerani na tunategemea kuendesha maisha yetu kupitia
uchuuzi huu mdogo mdogo na pia hatuna mtaji kwani tumejiajiri wenyewe serikali
ituangalie kwa kupitia hili,” alisema Chande.
Alisema wao
wanachangia pato la Taifa kupitia sekta hiyo kwa kulipa kodi pindi
wanaponunua bidhaa
mbalimbali madukani ikiwemo sukari, mchele, mafuta ya kula, ya taa,
sigara na nyinginezo
ila bado wanasumbuliwa na serikali.
Kaanael Minja alisema
zoezi la kuwakamata wachuuzi ambao hawakulipa leseni lililoendeshwa wiki
iliyopita, halikufanyika kwa haki kwani kuna baadhi yao waliporwa madini ambayo
siyo yao na hawakurudishiwa hadi hivi sasa.
“Kabla ya kuendesha
kamata kamata hiyo wangetoa elimu kwanza kwa wachuuzi hao lakini
kitendo cha kufika
kijiweni na kuanza kuwakamata watu wasio na leseni siyo kizuri, wangepaswa
kuwaelimisha kwanza,” alisema Minja.
Hata hivyo, mkuu wa
wilaya ya Simanjiro Mahmoud Kambona aliwataka wachuuzi hao kujipanga na kulipia
leseni ya ununuzi wa madini hayo ili waongeze mapato kwa serikali ambayo
inawaletea wananchi maendeleo.
“Wanatakiwa kutambua
kuwa hiyo ni sheria ambayo imepitishwa na sasa kinachotakiwa ni utekelezaji
kwani serikali zote hujiendesha kutokana na kodi ambazo zinalipwa na wananchi
wake na siyo vinginevyo,” alisema Kambona.
No comments:
Post a Comment