Askofu Pengo aridhishwa na huduma za afya zinazotolewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es salaam,Muadhama, Kardinali
Pengo amesema kwamba ameridhishwa na
huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), hivyo
itakuwa ni vigumu kwa Serikali kumshawishi kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Askofu Pengo ambaye amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo
katika hospitali ya MNH jiji Dar es Salaam kuanzia Januari Mosi, mwaka 2016 hadi sasa mara baada ya kuzungumza na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye alimtembelea leo mchana ili kuweza kufahamu maendeleo ya afya yake.
“Ninapenda kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania na kuwaondoa hofu kuwa hali ya Baba Askofu
Pengo imeimarika na anaendelea vizuri,
hajawekewa oxygen wala hajalazwa katika wodi ya uangalizi maalum(ICU) na ameridhika
na huduma zinazotolewa.
“Ameridhika na huduma zinazotolewa za moyo, itakuwa ni
vigumu sisi kama Serikali kumshawishi kwenda kutibiwa nje ya nchi, ”
alisema Waziri huyo.
Aidha Waziri Ummy alitembelea sehemu ya ICU, katika taasisi hiyo, ambapo
alisema operesheni ambazo ni ngumu zinafanyika, katika opresheni za moyo
kiwango cha kimataifa ni asilimia 6, wakati Tanzania imefikia kiwango cha
asilimia 4, hivyo tunafanya vizuri.
Aliongeza kwamba hatua hiyo inapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa
nje ya nchi, pia aliwataka hata wagonjwa kutoka taasisi binafsi kwenda kutibiwa
katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi alisema Baba Askofu huyo ameridhika na matibabu
aliyoyapata ambayo yanaweza kufanyika Tanzania, hivyo changamoto iliyopo kwa
Serikali kupitia wizara hiyo ni kuiwezesha taasisi hiyo kibajeti ili kuwezesha
wagonjwa anagalau 50 kati ya 300 ambao wako kwenye orodha ya kupatiwa huduma.
Aliongeza kwamba Baba Askofu huyo, ataruhusiwa siku za karibuni, baada ya
hali kuendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment