Dola za Marekani Milioni 132 kutumika mradi mkubwa wa umeme wa upepo wa Megawati 50 Singida. Kutoa ajira 2,200
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa akitoa
maagizo kwa Wakandarasi, Wataalamu kutoka
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Wizara ya Nishati na Madini na viongozi mbalimbali kwenye majumuisho ya ziara ya kamati hiyo, baada ya kufanya
ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Singida pamoja na kuzungumza na wananchi.
Na Greyson Mwase, Singida.
Mkuu
wa Kitengo cha Miundombinu na Nishati
kutoka Shirika la Maendeleo la
Taifa (NDC) Pascal Malesa amesema kuwa serikali inatarajia kutumia Dola za Marekani Milioni 132 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa
kuzalisha umeme wa upepo wenye uwezo wa
Megawati 50 ifikapo mapema mwaka 2016.
Malesa
aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ziara ya kutembelea mradi wa
kuzalisha umeme kwa njia ya upepo
unaojengwa katika eneo la Kisesile
nje kidogo ya Singida Mjini. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ipo mkoani
Singida kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea maendeleo yake
pamoja na kuzungumza na wananchi.
Alisema
mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati
ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)
lenye asilimia 60, Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lenye asilimia 20 na kampuni ya Power Pool
East Africa Limited yenye
asilimia 20 chini ya kampuni ya ubia iitwayo
Geo Wind Power Tanzania
Limited (Geo Wind) iliyoundwa mwaka 2011.
Malesa
alieleza kuwa gharama hizo zinahusisha utekelezaji wa mradi huo awamu ya kwanza kwa ajili ya kuzalisha
megawati 50 ambayo itahusisha ujenzi wa
msongo wa umeme wa kilovolti 220 umbali
wa kilomita 12 na kuunganisha kwenye
gridi ya taifa.
Alisema fedha hizo ni
mkopo kutoka Benki ya Exim
ya China na kuongeza
kuwa kwa sasa Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) linafuatilia mkopo
huu chini ya udhamini wa Serikali kupitia
Wizara ya Fedha baada ya kukamilisha vigezo vyote
vya mradi vilivyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kupata mkopo wa masharti nafuu na kuviwasilisha benki ya
Exim ya Serikali ya watu wa China.
No comments:
Post a Comment