Header Ads

Dkt Kigoda anastahili kupumzika jimbo la Handeni


 
 NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM.

UKWELI unauma. Na ili ufahamu hilo, mara nyingi watu wanaosema ukweli huwa hawapendwi. Watazushiwa na kusemwa mno kutokana na misimamo yao ya ukweli wanayosema mbele ya hadhira.

Wakati nasema haya, najipa moyo kuwa hata kama wapo watakaochukizwa na ukweli wangu, ila ipo siku jamii itaishi vizuri kutokana na kukombolewa na harakati za ukweli zinazoweza kupingwa na wachache wao waliokuwa kwenye nafasi mbalimbali za kiutawala.
Ndio, bora niseme tu Dkt Abdallah Omary Kigoda anastahili kupumzika kuongoza kama Mbunge wa Handeni, mkoani Tanga. Kigoda ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi CCM kwa miaka 20 sasa.

Kigoda aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kama mbunge mwaka 1995. Watoto waliozaliwa miaka ya 1995 mwaka 2015 wametimiza miaka 20. Ni kipindi kirefu mno kuongoza katika nchi inayojipambanua kuwa inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia.

Aidha, watoto hao waliozaliwa miaka ya 1995 na kukuta kero nyingi kama vile kukosa maji safi na salama, umeme vijijini, elimu duni, afya na mengineyo wanashangaa kama hadi leo kero hizo hazijatatuliwa ipasavyo licha ya kuongozwa na mbunge aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.
Kwanini Kigoda anastahili kupumzika? Licha ya Handeni kuwa wilaya kongwe na kubwa mno, lakini wananchi wake wanaishi maisha magumu na kuvumilia shida mbalimbali, jambo lililowachosha.

Wilaya hii haina maji. Wananchi wake wanalazimika kununua ndoo ya maji kwa Sh 700 hadi 1000 yanapotoka mbali zaidi. Kwa mtu mwenye familia ya watu wanne, atalazimika kununua ndoo tatu hadi tano. Endapo atanunua ndoo tano, basi atalazimika kulipia Sh 3500 kama atayanunua kwa Sh 700. Lakini kama atanunua kwa Sh 1000, basi mwananchi huyo atayanunua maji kwa Sh 5000. Je, pato lake kwa siku lipoje?

Mbaya zaidi, licha ya kuwa wilaya kongwe, lakini Hospitali ya wilaya ya Handeni haina chumba cha kuhifadhia maiti. Watu wanalazimika kupelekwa Hospitali ya wilaya Korogwe (Magunga) kuhifadhiwa kabla ya kuzikwa au kusafirishwa kwa wale wenye utaratibu huo. Aidha wilaya pia haina gari la kuzimia moto. Ulipotokea moto uliowatia hasara wananchi wengi, msaada ulizimika kutoka Korogwe. Hadi gari hilo lilipofika Handeni, moto huo ulishateketeza nyumba nyingi na kuwapa hasira wananchi kiasi cha kulipopoa kwa mawe gari hilo.

No comments:

Powered by Blogger.