BARABARA YA IGAWA – UBARUKU KUJENGWA KWA LAMI
Waziri wa Ujenzi Dkt. John
Pombe Magufuli amesema serikali itajenga barabara ya Igawa hadi Ubaruku KM 18
kwa kiwango cha lami ili kuinua fursa za uchumi za wilaya ya Mbarali na
kuwezesha magari makubwa kupita kwa urahisi kufuata mazao katika eneo hilo.
Waziri Dkt. Magufuli amesema
hayo katika ziara yake inayoendelea mkoani Mbeya ambapo leo ameweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya igawa-ubaruku yenye urefu wa KM 18 na kusisitiza barabara
hiyo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
“Nitahakikisha barabara
hii inajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika mapema ili kuunga mkono juhudi
za wananchi wa Mbarali wanaotekeleza sera ya kilimo kwanza kwa kuzalisha mpunga
na mahindi kwa wingi”, amesisitiza waziri Magufuli.

Amemwagiza Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Barabara Nchini TANROADS Eng. Patrick Mfugale kufanya usanifu ili
kuwezesha madaraja kumudu kupitisha magari yenye uzito wa tani 40
yatakayochukua mazao katika maeneo ya Rujewa na Ubaruku.
Eng. Mfugale amesema
barabara ya Igawa-Ubaruku kwa sasa ni barabara ya mkoa na ujenzi wake
utazingatia vigezo vya barabara za mikoa ili kukidhi mahitaji ya uzito wa
magari yatakayopita katika barabara hiyo.
Kuhusu barabara ya Igawa –Madibira
yenye urefu wa KM 153 ambayo upembuzi yakinifu na usanifu wake umekamilika waziri
Magufuli amesema Serikali inatafuta fedha ili kuijenga barabara hiyo kwa
kiwango cha lami na hivyo kuifungua kiuchumi wilaya ya Mbarali.
Amesisitiza umuhimu wa
umoja,mshikamano na uaminifu kwa wananchi wa Mbarali na kuwataka vijana
watakaopata kazi wakati wa ujenzi wa barabara hiyo kuwa waaminifu.
Naye mkuu wa mkoa wa Mbeya
Abbas Kandoro amemshukuru Waziri wa Ujenzi kwa kuamua kujenga kwa lami barabara
za Mpemba hadi Isongole wilayani Ileje ,Igawa hadi Ubaruku wilayani Mbarali na Kikyusa
hadi Matema wilayani Kyela na kusisitiza barabara hizo zitakapokamilika zitaimarisha
usafiri na kuibua fursa za ajira na uchumi kwa wakazi wengi wa mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment