TAARIFA YA MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO (CHADEMA),JOHN MNYIKA KWA DAWASA NA DAWASCO
Katika
kutekeleza kazi ya mbunge ya kuisimamia Serikali itakumbukwa kwamba tarehe 12
Mei 2014 nilichukua hatua bungeni ya kutaka Serikali kutatua kwa dharura
matatizo katika mtambo wa maji wa Ruvu Juu yenye kukosesha maji kwa wananchi wa
Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani.
Nilitaka
kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2013,
Waziri wa Maji Prof Jumanne Maghembe atoe kauli bungeni juu ya matatizo ya maji
katika maeneo yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo kwa kuweka bayana
iwapo kuna hujuma na kurejesha kwa haraka huduma kwa wananchi.
Kufuatia
hatua hiyo hali ya upatikanaji wa maji iliongezeka katika maeneo machache ndani
ya siku chache lakini kwa sasa katika maeneo mengi yanayohudumiwa na mabomba
kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu katika kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois,
Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi matatizo ya maji yamejirudia.
Katika
kuendelea kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali
natoa mwito wa wazi kwa wenyeviti wa bodi za Wakurugenzi na Maafisa Watendaji Wakuu
wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar
Es Salaam (DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ndani ya siku
tatu kusimamia kazi ya dharura kuhusu matatizo ya mtambo wa maji wa Ruvu Juu
yanayoendelea mpaka hivi sasa.
Aidha,
ndani ya siku hizo tatu wajitokeze mbele ya vyombo vya habari kutoa maelezo kwa
umma kueleza kwanini mpaka sasa huduma ya maji katika maeneo mengi katika Jimbo
la Ubungo na Jiji la Dar Es Salaam kwa
ujumla yanayohudumiwa na mabomba yanayotoka katika mtambo wa Ruvu Juu hayapati
huduma ya maji inavyostahili na lini matatizo yaliyopo yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa
upande mwingine, ndani ya muda huo huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maji ajitokeze mbele ya vyombo vya habari na kueleza umma matokeo ya uchunguzi
uliopaswa kufanyika ndani ya mwezi mmoja kubaini kama matatizo ya mara kwa mara
ya Mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa mengine ya kibinadamu.
DAWASA,
DAWASCO na Wizara ya Maji wasipojitokeza ndani ya siku tatu mbele ya vyombo vya
habari kutoa maelezo kwa umma nitachukua hatua za kibunge nitakazoona zinafaa
dhidi ya Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kwa kulidanganya Bunge kupitia
kauli ya Serikali aliyotoa Bungeni mwezi Mei 2014.
Ikumbukwe
kwamba tarehe 12 Mei 2014 ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa mbunge wa
kuwawakilisha wananchi nilieleza Bunge kwamba matatizo katika mtambo wa Ruvu
Juu yamekuwa yakijirudiarudia kwa nyakati mbalimbali kwa kipindi cha takribani
miezi mitatu kati ya Januari mpaka Mei 2014 katika maeneo ambayo awali yalikuwa
yakipata mgawo wa maji.
Nilichukua
hatua hiyo kwa niaba ya wananchi wanaohudumiwa na mtambo huo katika kata za
Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi kwenye Jimbo la Ubungo; na kata mbalimbali za
majimbo ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Segerea nk.
Kufuatia
hatua hiyo, Mwezi Mei 2014 Waziri wa Maji Prof. Maghembe alitoa kauli ya
Serikali ya kueleza matatizo yanayoukabili mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu
kwa ajili ya Jiji la Dar es salaam na maeneo ya DAWASA katika mkoa wa Pwani.
Katika
kauli yake Waziri Maghembe alikiri kwamba kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe
01.03.2014 na tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango na
kufikia kati ya lita milioni 8.2 na lita milioni 57.4 ikilinganishwa na lita
milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo.
Katika
kauli yake bungeni, Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa Ruvu Juu
kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60),
kukatika kwa Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana (turbidity)
wakati wa mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na
husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu wa upatikanaji wa vipuri
halisi (genuine parts). Hata
hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala kukanusha juu ya madai ya kuwepo kwa
udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma katika mitambo ya vyanzo vya maji na
mitandao ya mabomba ya maji.
Waziri
Maghembe alieleza Bunge kwamba Wizara imechukua hatua za kutatua matatizo
yaiyopo kwa kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana zilizopo hapa
nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jeshi, kuagiza vipuri nje ya nchi na kutoa
matangazo kwa wananchi kuhusu upungufu wa maji pale uzalishaji
unapopungua/kusimama.
Waziri
Maghembe alilieleza bunge kwamba baada ya hatua hizo uzalishaji wa Maji wa
Mtambo wa Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya kawaida na kutoa mfano
wa kwamba tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa maji ulikua lita milioni 80.3 kwa
siku. Aidha,
Waziri Maghembe alitoa kauli Bungeni kwamba Wizara ya Maji imeunda Kamati
Maalum ambayo imeanza kufanya tathmini ya kina juu ya chanzo cha matatizo ya
mara kwa mara katika mtambo wa kusafisha maji wa Ruvu Juu.
Waziri
Maghembe alieleza kwamba kamati hiyo itafanya uchunguzi kubaini kama matatizo
hayo yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa ya binadamu na
kuahidi kwamba kamati itatoa taarifa yake katika kipindi cha mwezi mmoja. Mwezi
mmoja umepita tangu nilipohoji bungeni tarehe 12 Mei 2014, hivyo ni wakati
muafaka kwa mamlaka zote zinazohusika kuweza kutoa mrejesho juu ya uchunguzi
huo na hatua nyingine za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi kama
nilivyozieleza katika hoja binafsi niliyoiwasilisha bungeni kwa niaba ya
wananchi tarehe 4 Februari 2013.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment