HIKI NDICHO WALIVYOFANYA YANGA KWA PRINSON UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR ES SALAAM JANA.
DAR ES SALAAM.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu,
Yanga jana waliichakaza Prisons kwa mabao 5-0, lakini hawakuweza kushika
usukani baada ya Azam kuendelea kujichimbia kileleni kwa kushinda 2-0
dhidi ya Mgambo Shooting.
Mshambuliaji Hamisi Kiiza alitokea benchi na
kufunga mabao mawili, huku Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa na Nadir Haroub,
aliyefunga kwa penati, wakihitimisha ushindi huo mnono.
Ushindi huo wa Yanga unaendeleza rekodi yake nzuri
ya kutoa vipigo vikubwa msimu huu baada ya kuinyuka Ruvu Shooting 7-0
na Ashanti United (5-1).
Pamoja na ushindi huo, Yanga imebaki nafasi ya
pili ikiwa na pointi 46, wakati mabao ya John Bocco na Briany Omony
yalitosha kuiweka Azam kileleni kwa kufikisha pointi 50.
Yanga waliuanza mchezo huo kwa kasi na dakika 16
beki wa Prison, Nurdin Chona nusura ajifunge wakati akijaribu kuokoa
shambulizi.
Okwi aliwainua mashabiki wa Yanga katika dakika 20
kwa kufunga bao la kuongoza kwa mpira wa adhabu akiwa nje mita 18.
Alipiga kiki na mpira kumshinda kipa Beno Kakolanya baada ya mpira huo
kumgonga kidogo kiungo wa Prisons, Jumanne Elfadhil.
Kocha wa Yanga, Han Van Pluijm alimtoa Jerryson
Tegete dakika 33 na kumwingiza Hussein Javu na mabadiliko hayo
yaliiongeza nguvu safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao.
Mwamuzi Andrew Shamba aliizawadiwa penalti Prisons
dakika 34 baada ya beki wa Yanga, Oscar Joshua kumwangusha kwenye eneo
la hatari mshambuliaji Frank Hau. Hata hivyo, Prison walipoteza penalti
hiyo baada ya mkwaju wa Lugano Mwangama kupaa juu ya goli.
Baada ya tukio hilo Yanga waliamka na kuanza
kulishambulia kama nyuki lango la Prisons na dakika 38 krosi ya Javu
ilimkuta Ngasa ambaye alipachika bao la pili.
Javu alikosa bao dakika 44 baada ya shuti lake
kugonga mwamba na mpira kurudi uwanjani kabla ya Ngasa kupoteza nafasi
ya kufunga dakika 45 na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa
mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Prisons walimtoa Ibrahim Mamba
na kumwingiza Six Mwasekaga wakati Yanga walimpumzisha Okwi na kuingia
Kiiza dakika 59.
Kiiza, ambaye alipoteza penalti katika mechi dhidi
ya Azam wiki iliyopita, alisahihisha makjosa yake alipowainua mashabiki
wa Yanga dakika 67 kwa kupachika bao la tatu akiunganisha vizuri krosi
ya Simon Msuva.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment