Megawati 150 kuongezeka katika Gridi ya Taifa
Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji Mhandisi Decklan Mhaiki (katikati) akimweleza Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
(kushoto) pamoja na Waandishi wa habari moja ya mashine za kufua Umeme
zitakazofungwa katika eneo la Kinyerezi
I jijini, Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi huo, Bw.
Shaun Moore.
Mmoja wa mitambo ya kufua umeme ambao utafungwa
katika eneo la Kinyerezi I mara baada ya ujenzi kukamilika. Mitambo hiyo,
inatarajiwa kuzalisha kiasi cha megawati za umeme 150 ambazo zitaunganishwa
katika gridi ya Taifa.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji kutoka TANESCO, Wizara ya
Nishati na Madini na watumishi wa kampuni inayojenga kituo hicho ya Jacobsen
Elektro.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo akimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi wa kituo cha Kinyerezi
I, Bw. Shaun Moore, wakati akimweleza maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
======== ======== ======
Megawati 150
kuongezeka katika Gridi ya Taifa
Na Asteria Muhozya na Jema Marko, Dar es Salaam
Megawati 150 zinatarajiwa kuongezeka katika gridi ya
Taifa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme eneo la
Kinyerezi I pamoja na kukamilika kwa ufungaji wa mitambo hiyo, ambapo shughuli
zima inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba mwaka 2014.
Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo wakati
akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo
hicho alieleza kuwa kukamilika
kwa ujenzi wa kituo hicho ni hatua mojawapo ya kutimiza azma ya Serikali ya kuongeza umeme katika gridi ya
Taifa.
Aidha, aliwataka watanzania na wateja wa umeme kujenga
imani na Shirika la Umeme Tanzania kutokana na mabadiliko ambayo tayari
yamefanyika katika shirika hilo ikiwemo utekelezaji wa mipango mbalimbali ya
kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika.
“Nataka Watanzania muelewe kuwa, Tanesco ya sasa sio kama ya zamani. Umeme
utapatikana. Kampuni ya Jacobsen Elektro ambao wanafanya kazi ya ujenzi ni
wazoefu katika shughuli hizi, tuna imani kazi itakwenda vizuri kama
tulivyopanga. Tanesco itatatua tatizo la umeme”. Alisema Waziri Muhongo.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alieleza kuwa, asilimia 98 ya kampuni za
kitanzania kupata kandarasi katika
ujenzi huo ni fursa mojawapo ambazo watanzania wanatakiwa kuzitumia katika
kipindi hiki ambacho nchi inaingia katika uchumi wa gesi.
Akizungumzia kuhusu fedha za ujenzi wa kituo cha kinyerezi I na ujenzi wa
vituo vingine vya kinyerezi II, III na IV, Waziri Sospter Muhongo alieleza
kuwa, fedha za ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I zimetolewa
na Serikali kupitia TANESCO. Ujenzi wa
kituo cha kinyerezi II fedha itatokana
na ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japani , wakati ujenzi wa
kinyerezi III na IV fedha zitatokana na kuingia ubia kati ya Serikali na kampuni ya Kichina.
Wakati huo huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji, wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Decklan Mhaiki, aliongeza kuwa,
katika kituo hicho zitafungwa jenereta nne ambapo kila moja itakuwa na uwezo wa
kuzalisha kiasi cha megawati 37.5, hivyo kufanya jumla ya megawati 150 kutoka
kituo hicho.
Vilevile, alieleza kuwa, katika jitihada za kuhakikisha kwamba Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) linatatua tatizo la Umeme nchini, tayari shirika hilo na
mkandarasi anayejenga kituo hicho, kampuni ya Jacobsen Elektro wameanza
mazungumzo ili kuongeza kiasi kingine cha megawati 200 ili kituo cha kinyerezi I
kiweze kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 350.
Akielezea kuhusu ubora wa jenereta zitakazofungwa kituoni hapo, Mhaiki
alieleza kuwa, generator hizo ni za kisasa na hazina athari za kimazingira
ikiwemo kelele.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Jacobsen
Elektro, Bw. Shaun Moore, akielezea
maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, alieleza kuwa, ujenzi wa kituo hicho
unaendelea vizuri kutokana na kampuni hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri
na kampuni za kitanzania zilizochukua kandarasi tofauti tofauti za ujenzi wa
kituo hicho, ambapo takriban asilimia 98 ya kandarasi na wafanyakazi ni kutoka kampuni za kitanzania.
No comments:
Post a Comment