IPTL kusaidia miradi ya kuwawezesha vijana kiuchumi
Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL), Bw. Harbinder Signh Sethi (kushoto) na Katibu na
Mwanasheria Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Joseph Makandege (wapili kushoto)
wakikabidhi hundi ya shilingi milioni 11 kwa mwakilishi wa Kanisa la Mt.
Rita Wakashia lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, George Kashushura.
Fedha hizo zitatumika kuanzisha SACCOS ya kanisa hilo, lenye lengo la
kuwainua vijana kiuchumi. Makabidhiano hayo yalifanyika jijini Dar es
Salaam jana
====== ======= =======
IPTL kusaidia miradi ya kuwawezesha vijana kiuchumi
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL) imeanza utekelezaji wa mpango wake wa kuiwezesha miradi mbali
mbali inayowawezesha vijana wakitanzania kuimarika kiuchumi, ikiwa na
lengo la kukuza maendeleo ya uchumi nchini.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 11 kwa kikundi cha
kwaya cha kanisa la Mtakatifu Rita Wakashia lililopo Kimara jijini Dar
es Salaam, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Bw. Harbinder Singh Sethi
alisema kampuni yake imejidhatiti katika kuhakikisa inatekeleza mipango
yake ya kupiga jeki miradi ambayo itasaidia kuondoa umasikini na ukosefu
wa ajira miongoni mwa vijana nchini Tanzania.
“Hizi
milioni 11 tulizotoa kwa Kanisa la Mt. Rita Wakashia, ambazo zitatumika
katika uanzishwaji wa SACCOS kwa wanakwaya wa kanisa, ni sehemu ya
utekelezaji wa mpango wetu wa kuchangia katika kusaidia miradi ya
kijamii na ya kiuchumi unaolenga kusaidia vijana wa kitanzania kuwa
wachangiaji wakubwa katika ukuaji wa uchumi nchini,” alisema Singh.
Bw.
Harbinder alisema mpango huo pia unalenga kusaidia mashule, makanisa,
misikiti na makampuni mengine yasiyotengeneza faida yanayofanyakazi ili
kuwawezesha vijana kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya
kiuchumi Tanzania.
“Tunaamini
kuwa SACCOS hii itakayoanzishwa itatoa fursa nzuri ya kujiwekea akiba
nakutumika kama chanzo cha mikopo kwa vijana na wanakwaya wengine wa
kanisa. Hii ni hatua kubwa katika kujikwamua kiuchumi katika jumuiya hii
ya kanisa, ambayo ni taasisi isiyotengeneza faida,” alisema.
Naye
Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL, Bw. Joseph Makandege alisema ili
kuwapa sauti vijana na kuwaongezea fursa za kujiimarisha kiuchumi, IPTL
kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Power (PAP) imetenga sehemu
ya pato lake kwa ajili ya kupiga jeki miradi ya maendeleo ya kijamii,
kwa dhamira ya kusaidia miradi ya kimaendeleo inayowalenga vijana.
“Sisi
kama IPTL na PAP, tumeona kuwa ni jukumu letu kuisaidia jamii
inayotuzunguka. Kwa kuanzisha SACCOS, ninaimani vijana wa kanisa la Mt.
Rita Wakashia wataweza kuanzisha mradi madhubuti utakaowaletea
mabadiliko chanya ya kiuchumi. Hii ndiyo sababu tulishawishika kutoa
mtaji huu wa kuanzia ili kuwawezesha kuanzisha SACCOS,” alisema Bw.
Makandege.
Akizungumza
kwa niaba ya wanakwaya na waumini wengine wa kanisa hilo, Bw. George
Kashushura alizishukuru IPTL na PAP kwa msaada wao na kubainisha kuwa
fedha iliyotolewa itaelekezwa katika malengo mazuri yatakayobadilisha
maisha ya vijana walio wengi.
“Fedha
tulizopokea leo hii zitatumika kama mtaji wa kuanzisha SACCOS yetu ya
kanisa ambayo itakuwa ni chachu ya mabadiliko ya maisha ya vijana walio
wengi katika kanisa letu,” alisema Kashushura.

No comments:
Post a Comment