Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Afisa Habari wa
Jeshi la Kujenga Taifa Meja Emmanuel Mluga(Kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi
wa habari (hawapo pichani) na kuwataka kuelimisha Umma juu ya umuhimu wa vijana
kujiunga na mafunzo ya JKT,wakati wa Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Idara
ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia Ni Afisa Habari wa Idara ya
Habari (MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.Picha na Hassan Silayo - MAELEZO
Msemaji wa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Luteni Kanali Juma Sipe(Kushoto)
akieleza kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) Mpango wa Serikali Kupitia
Wizara hiyo Kuendelea Kuboresha Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria,wakati wa Mkutano
uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es
Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Emmanuel Mluga.
======= ===== =====
Wizara
ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria
Wizara
ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Hatua hii inafuatia kurejeshwa upya kwa mafunzo hayo kama Serikali ilivyokuwa
imeahidi.
Mafunzo
hayo yaliyoanza mapema 2013 yanatarajiwa kuwahusisha vijana 41,341 waliomaliza
kidato cha sita katika shule mbali mbali nchini. Katika awamu ya kwanza vijana 5,000 (12%) walitakiwa kuhudhuria mafunzo
kwa muda wa miezi mitatu
kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Juni 2013.
Awamu
ya pili ya mafunzo hayo iliyoanza mwezi Juni JKT ilitarajiwa kuchukua vijana 10,000 (24%) na kumaliza mafunzo yao
mwezi Septemba 2013. Katika awamu ya
tatu itakayoanza mwezi Oktoba 2013 JKT itachukua vijana 15,000 (37%). Aidha, awamu ya nne JKT itachukua vijana
11,341 (27%) mwanzoni mwa Januari 2014 na vijana hao watamaliza mafunzo mwezi
Aprili, 2014 na hivyo kukamilisha idadi ya vijana waliomaliza kidato cha sita
kwa mwaka 2013.
Utoaji
wa mafunzo haya kwa miezi mitatu mitatu unafuatia maagizo ya Serikali kwani kwa
muda wa miezi sita iliyokusudiwa wakati wa kurejesha mafunzo hayo ni wazi
vijana wengi wasingepata fursa hiyo adhimu.
Changamoto
kubwa zinazolikabili JKT ni pamoja na hofu wanayokuwa nayo wazazi kutokana na
visingizio wanavyopewa na vijana baada ya kuwasili makambini. Tunawaasa wazazi
kutojengewa hofu kwa taarifa zisizo rasmi wanazopewa na watoto wao kwani Wizara
ilizifanyia kazi hofu zilizoelezwa na vijana na kubaini kuwa hazina ukweli. Kwa
mfano, mtoto anadai kuwa anaumwa na hapati matibabu, lakini tunapofuatilia
tunamkuta yupo kwenye gwaride (mzima wa afya. Chakufurahisha baadhi ya vijana
hao hao wakati wa kumaliza mafunzo wamekuwa hawana haraka tena ya kuondoka
makambini!
Pili,
lipo tatizo la kukwepa mafunzo (dodging). Mfano katika awamu ya kwanza
tulitarajia kupokea vijana 5,000 lakini waliojitokeza ni 4,712 (vijana 288
wakiwa wamekwepa mafunzo). Katika awamu ya pili kati ya vijana 10,000 ni vijana
9,510 tu ndio waliojitokeza, (watoro 490). Tunapenda kuwahakikishia wote
wanaokwepa mafunzo kuwa wataendelea kufuatiliwa na mara watakapopatikana hatua
za kuwarejesha katika mafunzo zitachukuliwa.
Changamoto ya tatu ni kutopatikana kwa huduma za mtandao
(internet) makambini. Wizara inatambua umuhimu wa mtandao na hivyo juhudi
zitafanyika siku za usoni kuyaunganisha makambi kwa kadri mkonga wa Taifa
unavyozidi kuenea nchini. Hata hivyo, kijana anayekuwa mafunzoni kwa miezi
mitatu atajikuta hana muda wa kutumia huduma hiyo kutokana na majukumu
aliyonayo. Kwa wanaoomba nafasi vyuo vya elimu ya juu upo utaratibu wa
kuwaruhusu kutumia huduma zilizo nje ya makambi.
Aidha, JKT linakabiliwa pia na changamoto ya kutoa
mafunzo kwa muda mrefu zaidi kutokana na maombi ya vijana wanaomaliza na pia
maombi ya waheshimiwa wabunge. Hii ni ishara njema ya kuona umuhimu wa mafunzo
yanayotolewa na kwa kadri makambi yatakavyoongezeka nchini suala la muda wa
mafunzo pia litaangaliwa.
Changamoto nyingine ni miundombinu michache ikilinganishwa
na idadi kubwa ya vijana wanaotarajiwa kumaliza kidado cha sita na vyuo kila
mwaka. Suluhisho la jambo hili litapatikana baada ya kupanuliwa kwa makambi ya
JKT.
Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi ili kuwa na mpango utakaohakikisha vijana wanaofaulu vizuri
wanapata mafunzo mapema na kuwawezesha kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa
wakati. Kwa wale wanaojiunga sasa na ambao tayari wamedahiliwa, Wizara
imewasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kupata orodha yao na
hatimaye kuwawekea utaratibu wa kujiunga na mafunzo hayo baada ya kumaliza
masomo yao.
Imetolewa
na Luteni Kanali Juma Nkangaa Issa Sipe,
Msemaji,
Wizara ya Ulinzi na JKT,
Simu:
0756448787/0655878744/0784370500/0772516666.
No comments:
Post a Comment